Siku sita kabla ya maadhimisho ya
Siku ya Wanawake Duniani, mwanamke mmoja amenusurika kuliwa na mamba wakati
akiteka maji kwenye Mto Mgeta, Dakawa mkoani Morogoro, ikiwa ni madhara
yanayotokana na kukosekana kwa huduma hiyo muhimu katika kijiji anachoishi.
Martha Malambi (25), baada ya
shambulio hilo la Februari 17 lililosababisha kumpoteza mtoto wake wa kiume,
Godfrey David (mwaka mmoja na miezi miwili) ambaye alikufa na baadaye maiti
yake kusombwa na maji, kwa sasa anaendelea na matibabu katika Taasisi ya
Mifupa na Mishipa ya Fahamu Hospitali ya Muhimbili (MOI).
Ni saa 11:00 jioni katika kijiji
cha Ukutu, Kata ya Bwakilachini, Martha akiwa amembeba mwanaye mgongoni,
anafika katika Mto Mgeta baada ya kutembea mwendo wa nusu saa akitafuta maji
“Nilikwenda mtoni kuchota maji
nikiwa nimembeba mwanangu, baada ya kujitwisha kichwani wakati naanza kutoka
mtoni mamba mkubwa alinivamia kwa nyuma, alinikamata mguu sehemu ya msuli na
paja akanivuta mtoni,” anasimulia Martha aliyepambana kijasiri na mamba huyo.
Anasema baada ya kudondoka mamba
huyo alimvuta mpaka mtoni kwenye kina kirefu kisha kumzamisha chini ya maji,
“Nilimhisi mwanangu namna alivyohangaika na maji aliyokuwa anakunywa baada ya
sekunde chache alituibua tena juu hapohapo kitenge kikafunguka na mtoto
akaondoka na maji, nilipata uchungu mkubwa,” anasema.
Anasema mamba alizidi kumbana
zaidi na kumvutia bondeni. Wakati wa purukushani hizo alikuwa amembana mguu
kwa meno yake na kuacha kiwiliwili, hivyo akawa anapiga kelele kuomba msaada
huku akiendelea kupambana naye.
Mama huyo wa watoto wawili, huku
mmoja aliyemuacha nyumbani akiwa na umri wa miaka mitano, anasema alitumia
nguvu zaidi kupanua mdomo wa mamba ili kumpa maumivu, lakini aliendelea
kumshinda nguvu kutokana na urefu wa mnyama huyo kuwa maradufu ya urefu wake
“Kutokana na purukushani ile,
aliona hajanidhibiti vizuri kwa sababu alinishika mguu mmoja, akajaribu
kusogea kwenye kina kifupi cha maji ili anikamate vizuri,” anasimulia Martha.
Anasema hatua ya mamba huyo
kusogea kwenye kina kifupi cha maji ya mto kutoka kina kirefu, kilimsaidia
kuyafikia matete (magugu maji) hivyo aliyashika na kuyang’ang’ania kwa nguvu
huku akiomba msaada kwa kupiga kelele.
Mwanamke huyo anasema ilikuwa
bahati kwake, kwani kulikuwa na wavulana ambao hawakuwa mbali na mto huo
ambao walisikia kelele za kuomba msaada na kuwahi eneo hilo, wawili wakiwa na
magongo wawili wengine mapanga hivyo kuingia kwenye maji na kuanza
kumshambulia mamba huyo.
Pamoja na msaada huo wa watu,
mamba aliendelea kung’ang’ania mguu wake lakini mashambulizi yalivyozidi
mamba alionekana kuchoka na kupata maumivu, hivyo kuuachia mguu na kuzama
majini.
Hata hivyo, Martha anasema kabla
hajaokolewa alikata tamaa kwani alihisi tayari amekufa: “Yule mamba mkubwa
karibu mara mbili ya mwili wangu aliniogopesha sana, sikuwa nimewahi kumuona
kwa macho yangu kabla ya siku hiyo. Viboko nawajua vizuri kwa sababu nimewahi
kuwaona mara nyingi kijijini
“Wale vijana walinichukua na
kunipeleka nchi kavu baadaye Zahanati ya Lukumi, ambako walinipatia huduma
usiku kucha, asubuhi ya Februari 18 walinisafisha vizuri maeneo yote
yaliyoathiriwa na kucha na meno ya mamba huyo.”
Anasema kutokana na ukubwa wa
majeraha hayo na mguu kuvunjika, alihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro
ambako baada ya kuhudumiwa takriban siku tano walimweleza kuwa tatizo lake
inabidi apelekwe Muhimbili. Safari yake kwenda MOI ilianza akiwa yeye na
wauguzi tu, alipofika alipokelewa na kupelekwa chumba cha upasuaji ambako
alirekebishwa maeneo ya nyonga ambayo pia yaliathiriwa
“Nimefika MOI nikiwa peke yangu.
Sina ndugu hapa Dar es Salaam wala ndugu yeyote kutoka nyumbani ambaye
amefika hospitali tangu siku hiyo. Nashukuru wauguzi na madaktari wamekuwa
wakinisaidia wakati wote, ninapata matibabu vizuri, ninapata chakula,
nashukuru kwa hilo” anasema na kusisitiza kuwa familia yake ni maskini, hivyo
hana mawasiliano nao kwani simu aliyoitegemea ilisombwa na maji.
Uhaba wa maji Ukutu
Martha anayeishi na wazazi wake
kijijini hapo, anasema hawawezi kuepuka kufuata maji mtoni kwa kuwa hakuna
chanzo kingine cha maji kijijini zaidi ya mto Mgeta, miaka yote wamekuwa
wakichota maji hapo.
Miaka yote tuliyoishi pale
hatujawahi kusikia tukio la shambulio la mamba eneo hilo. Nimezaliwa na
kukulia hapo na wazazi wangu pia wamezaliwa na kukulia hapohapo. Wanyama wapo
kwenye huo mto, hasa viboko, maji yakijaa wanatembea hadi kwenye makazi ya
watu lakini mamba hawakuwahi kuwapo eneo hilo zaidi na maeneo ya mbali,”
anasema.
Martha ambaye ni mkulima wa mpunga
na mahindi anaainisha kuwa miaka kadhaa iliyopita, kulikuwa na mabomba matatu
ya jumuiya katika kijiji chao lakini kwa zaidi ya miaka minne sasa hayafanyi
kazi tangu yalipoharibika.
kumfanyia upasuaji
Daktari bingwa mwandamizi wa
upasuaji mifupa MOI, Paul Marealle anathibitisha kumpokea Martha na kwamba,
tayari wameanza kumpatia matibabu kinachosubiriwa ni upasuaji
“Alipata jeraha kubwa la kuvunjika
mfupa wa paja na vidonda kwenye eneo la paja na mguu wa kulia,” anasema Dk Marealle
na kuongeza:
“Wagonjwa wengi wa namna hii
wanakuwa wamepoteza damu, hivyo tunawaongezea na tunawapatia huduma ya karibu
kabisa, kwa sasa tumemtibu na majeraha yake yamepona, kwa hivyo tutamrudisha
chumba cha upasuaji kushughulika na mfupa wake ambao umevujika
“Tunajaribu kuondoa uchafu na sumu
yote ambayo inaonekana kwa macho na wanawekwa kwenye antibiotic maalumu na
kurudishwa chumba cha upasuaji mara kwa mara
Huduma kwa majeruhi wa mamba
Anasema huduma ya kwanza ambayo
mgonjwa aliyeng’atwa na mamba anafaa kupewa ni kuzuia damu isitoke, kwa kuwa
hupoteza damu nyingi huku akisisitiza majeruhi yeyote lazima aangaliwe kwa
namna anavyobebwa na kuhudumiwa kulingana na majeraha yake
“Mamba anakula vitu vingi hivyo
ana sumu kali ya vijidudu vinavyokaa kwenye meno yake vinavyotokana na
uchafu, kwa hivyo kitu cha kwanza lazima kuhakikisha kidonda kimesafishwa
vizuri hata na maji yanayotiririka,” alisema.
Dk Marealle anasema iwapo mgonjwa
asipopewa tiba ya antibiotic kwa haraka, kinachoweza kutokea ni kufa kwa
ngozi, misuli na mishipa ya fahamu hivyo madhara yake ni kukatwa sehemu
husika.
|
|
MAMA APAMBANA KUJIJITETEA KWENYE MENO YA MAMBA MWANAE AFARIKI
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 02, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment