Lekoko Lepilal"Ardhi ipimwe Arumeru tuondokane na umaskini na uuzaji wa Ardhi.


Hivi karibuni nilihudhuria mkutano wa Halmashauri kuu ya CCM wilaya Arumeru wakiwemo wataalam wa Arusha DC, Mkurugenzi na DC wa Monduli anayekaimu Wilaya Arumeru kwa sasa.
Lengo la mkutano huo ni kuangalia ni kwa kiasi gani chama chamapinduzi (CCM) kimetekeleza ila yake mwaka wa 2017/2018.

Kusema kweli nilifarijika kwa kiasi kikubwa maana mambo mengi yamefanyiwa kazi japo yapo mambo ambayo yangetakiwa kufanyiwa kazi kwa kuangalia ualisia wa maisha ya watu wa Arusha DC/Arumeru Magharibi. “tunahitaji ku-localize content inapoofikia utekelezaji wa ‘miradi’ kwenye maeneo ili kuleta impact pana maana ilani inaangalia taswira ya nchi kwa mapana yake”. My take!

Lakini kwa ujumla nilipata faraja kwa utekelezaji kwani halmashauri imejitahi kusimamia vema pesa zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kama maji, afya, barabara, uwezeshwaji nk!

Lengo langu la kuandika makala haya ni kutaka Halmashauri yetu Arusha DC ijitahidi sana ili watu wetu wasaidiwe ardhi ipimwe waondokana na uuzaji wa ardhi kama chanzo cha mapato, waondokane na migogoro, waondokane na umaskini kwa kunyakua fursa zinazoanza kujitokeza kama hizi za riba nafuu kutoka kwenye mabenki na sekta za kifedha nchi.

Ilani ya CCM ibara ya 37 inayosema: Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Chama Cha Mapinduzi kitaielekeza Serikali kuendelea kutekeleza mipango ya kuendeleza ardhi katika maeneo yafuatayo:
b)Utayarishaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya ardhi
nchini
(i) Kuendelea kutekeleza Mpango wa Taifa wa Matumizi ya
Ardhi
(ii) Kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 7,500 na
mipango ya matumizi ya ardhi ya Wilaya 25
(iii) Kukamilisha upimaji wa mipaka ya vijiji vyote nchini
(iv) Kuwapatia wananchi hatimiliki za kimila 2,500,000 pamoja na kujenga masjala za ardhi 250 katika ngazi za Wilaya na Vijiji na
(v) Kuwapatia wananchi hati miliki 2,000,000 pamoja na kusaji nyaraka nyingine za kisheria.

Kwenye Ilani hii Ibara ya 37 (b) kama halmashauri yetu Arusha DC iliweka pia malengo yake na imetekeleza kwa kiwango chake. Nia yangu natamani na kuhitaji kama mwananchi mkaazi wa Arusha DC/Arumeru Magharibi wananchi wapatiwe elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa hati Miliki za kimila na za Hati miliki za kisheria na kuomba serikali ituweke kwenye mpango mkakati wa upimaji wa ardhi unaoendelea nchini kwani kati ya eneo lenye migogoro na uuzaji wa ardhi ni Arumeru.

Naelewa kwanini kuna migogoro na uuzaji wa ardhi.
Migogoro: Migogoro hutokana na mipaka ya zamani iliyowekwa kutokana na matumizi ya ardhi kwa miaka ya zamani bila kuangalia ongezeka la watu na matumizi yenyewe. Kutofanyiwa marekebisho haraka pale Wilaya, majimbo, kata na vijiji vinavyogawanywa.

Umiliki wa ardhi wa familia na kutoweka mpango maalum wa matumizi,umilikishaji na mipaka na ‘mmliki’ yaani baba akifariki mafarakano hutokea kwa majirani, watoto, wajuu nk! Kuchelewa kwa mpango bora wa matumizi ya ardhi kwa miaka ya nyuma.

Uuzaji wa ardhi: Uuzaji wa ardhi umeanza kuonekana kama chanzo cha kipato. Umaskini unaongezeka kwenye jamii zetu huchangia watu kuuza ardhi. Shule, kwa kuwa watu wameona matunda ya elimu wapo tayari wauze ardhi mtoto aende shule. Ongezeko la watu, kwa kuwa watu wanaongezeka watu huuza ardhi wapate kianzio waende maeneo yenye nafasi kwa makazi. Kilimo na ufugaji, kutokana na maeneo mengi kutokuwa na rutuba kwa kilimo wala nafasi ya kufugia watu huuza ili wahamie maeneo yenye rutuba na kwa ajili ya ufugaji.

Rai yangu kwa serikali yangu hasa Arusha
DC/Mkurugenzi/Mwenyekiti wa halmashauri, wawekeze nguvu kubwa na kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya kuweka mpango mkakati wa kupima ardhi walau kata 10 kabla ya 2020 ili wananchi wetu watumie hati zao za ardhi kukopa mikopo yenye riba nafuu waweze kufanya biashara na kuwasomesha watoto wao ili waondokane na umaskini badala ya kuuza ardhi. 

Unajua mtu akitumia hati kukopa kuna uwezekano mkubwa wa kurudisha mkopo badala ya kuuza eneo maana sio rahisi kununua ardhi ukishauuza. Najua unaweza ukamkuta mtu hana kitu kabisa na mwanaye yupo mwaka wa pili chuo kikuu na anatakiwa ada na matumizi mengine na anaona ni bora kuuza kipande cha ardhi mwanaye amalizie shule, kitu ambacho ni chaguo jema ili asiwe amepoteza mali nyingi miaka 15 na kupoteza maisha ya mwanaye. Sasa ili wazazi wetu waondokane na hicho kikombe, tuiombe serikali itusaidie kupima ardhi tuwe na hati tukope maana mtu akisoma na kupata kazi anaweza kukomboa shamba la familia yake. Mifano hiyo ipo hai!

Sasa kwa kuwa serikali kuu imeanza utekelezaji wa ilani kwa vitendo kwa kurahisisha mikopo kwa taasisi za kibenki kwa kupunguza riba (BOT), benki nao wameanza mchakato wa kushusha riba hadi asilimia 6! Hii ni fursa kubwa kwa Watanzania kwani mzazi wako akiwa na hati ya eneo na kijana amesoma ni rahisi kuandika business plan na kwenda bank na kuchukua pesa na kuanza biashara kubwa au ndogo na kuanza kujiajiri, kutengeneza ajira kwa watu wengine badala ya kusbiri serikali. Nina hakika mazingira haya yangekuwepo kwa miaka ya nyumba tungekuwa mbali.

Natoa mfano mdogo sana, kama mtu una hati miliki ya ardhi yako na unaweza kukopa zaidi ya million 30 bank kwa miaka mitano, nini kitamnyima kijana kwenda kununua mashine 3 za kusaga na kukoboa mahindi na huku kuna umeme wa REA na kuhamia maeneo ya kilimo na kuanza kiwanda kidogo na kupaki au kuuza unga kwa bei nafuu na kuanza mradi wa kuku na masoko yako! Naombeni tuwawezeshe watu hasa vijana wanaosoma kwa pesa nyingi na wapo mtaani kwa kuwaelekeza kutumia rasrimali zao wenyewe waweze kujitegemea.

Naambatanisha uthibitisho wa taarifa ya kushuka kwa riba za kibenki.
 Kama ardhi haitatumika vema kwa kupima maeneo na kuwapatia watu hati miliki zao kama inavyofanyika maeno mengine tutababaki kuwa amaskini na madalali wa mashamba na viwanja. Kama hatutatumia fursa hizi zinazojitokeza kutokana na jithada za serikali pesa zitaendelea kuwa ngumu mtaani na matajiri wataendelea kuwa matajiri! Kama wataalam hawatawasaidia watu kuona fursa na kunyakua kwa kuwawezesha kuconnet the dot, tubaki walalamikaji na watazamaji. Arusha DC, tunataka ardhi yetu itusaidie tuondokane na umaskini na halmashauri ipate mapato maana itaweza kudai kodi kwenye maeneo yaliyopimwa. Inawezekana tukiamua! Hata ukitaka kuuza eneo lako kama limepimwa basi utauza bei ya Scania 3 badala ya bajaji!
Naomba kuwasilisha
Lekoko Piniel Levilal
Mwanahabari

Lekoko Lepilal"Ardhi ipimwe Arumeru tuondokane na umaskini na uuzaji wa Ardhi. Lekoko Lepilal"Ardhi ipimwe Arumeru tuondokane na umaskini na uuzaji wa Ardhi.   Reviewed by KUSAGANEWS on March 21, 2018 Rating: 5

No comments: