ZITO NCHI HAIWEZI KURUDI KWENYE MFUMO WA CHAMA KMOJA


Kiongozi wa chama cha Act Wazalendo Taifa Zitto Kabwe,  amewataka wanachama wa ACT Wazalendo kutotereka na hali ya siasa ambayo kuna ubinywaji wa demokrasia na kusisitiza kuwa nchi hii haiwezi kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja licha ya nguvu nyingi kutumika ya kuua upinzani.

Alisema kinachopaswa kufanyika ni kusimama imara na kupigania demokrasia ya kweli ambayo itawafanya watu kuwa huru na kufanya kile wanachokitaka bila ya kuvunja sheria za nchi.

Zitto ameyasema hayo leo Februari 28 mjini Shinyanga akiwa kwenye ziara yake ya kuimarisha chama alipokutana kuzungumza na viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho mjini humo, na kuwataka wasitetereke na uendeshwaji wa siasa hapa nchini na kuanza kuhama vyama hovyo bali wajipange kisaikolojia na kukijenga chama.

Alisema siasa za sasa  nchini Tanzania ni ngumu, hivyo wasikate tamaa kuendeleza mapambano ya kupigania demokrasia hapa nchini, pamoja na kuendelea kuulinda mfumo wa vyama vingi ambao ndiyo mkombozi kwa watanzania na waendelee kujipanga kugombea majimbo katika chaguzi hizo ukiwemo  uchaguzo mkuu wa mwaka 2020.

Zitto Kabwe alieleza kuwa kutokana na jambo hilo la kubinywa kwa demokrasia hapa nchini wanapaswa kujiandaa kisaikolojia kwenye chaguzi hizo na kutotishika na watu wanaohama vyama vya siasa, bali waanze kujipanga mapema namna ya kulinda wizi wa kura, kutafuta mawakala waaminifu pamoja na viongozi kutatua kero za wananchi.


“Tunataka chama chetu kiwe tofauti na vyama vingine vya upinzani kwa kutohama hama vyama kwa kuhofia uchaguzi mkuu ujao kuwa hawatopata kura wala uongozi, bali sisi tujipange kisaikolojia na kufanya kazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, ambao ndio wenye ridhaa ya kutupatia uongozi,”alisema.

Aliwataka viongozi wa chama hicho ambao walipewa ridhaa ya wananchi kwenye chaguzi zilizopita (2014-15) za serikali za mita,madiwani na ubunge wawatumikie wananchi ipasavyo kwa kutatua kero zao ili kuonyesha utofauti wa viongozi wa ACT na wa vyama vingine ili kuendelea kukiimarisha chama kwa wananchi.

Nao baadhi ya wanachama hao akiwemo Maarufu Hassani, walionyesha wasiwasi juu ya baadhi ya viongozi ambao walipata ridhaa kwenye chaguzi zilizopita (2014-15) kuwa kutokana na vuguvugu la kisiasa hapa nchini la kubinywa kwa demokrasia na chaguzi zinavyoendeshwa kuwa kuna uwezekano wa viongozi hao wasirudi 2020.

Katika ziara hiyo, Zitto alifanikiwa kuvuna wanachama wapya Tisa kutoka vyama mbalimbali vya siasa ambapo aliwapatia kiapo cha utii wa chama hicho ili kuendelea kukilinda na kukijenga chama kwa wananchi ambao ndio watawapatia ridhaa ya kushika nchi.


ZITO NCHI HAIWEZI KURUDI KWENYE MFUMO WA CHAMA KMOJA ZITO NCHI HAIWEZI KURUDI KWENYE MFUMO WA CHAMA KMOJA Reviewed by KUSAGANEWS on February 28, 2018 Rating: 5

No comments: