Siku mbili baada ya Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kuahidi kumsomesha Angela Akwilini, mdogo wa marehemu Akwilina aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), familia hiyo imetoa ombi lingine kwa Serikali.
Msemaji wa familia hiyo, Dismas
Shirima akizungumza na Mwananchi jana alisema, “Nampongeza waziri kwa kuona
umuhimu wa kuziba pengo la Akwilina kwa kumsomesha mdogo wake Angela
aliyekuwa akitegemewa kwa kiasi kikubwa katika familia.”
Shirima pia alimuomba Waziri
Ndalichako kumsomesha ndugu mwingine wa Akwilina aliyeacha shule akiwa kidato
cha tatu kwa kukosa mahitaji ya shule
“Waziri akifanya hivyo atakuwa
amepunguza machungu kwa familia hii maskini,” alisema.
Mtoto huyo, Yulia Akwilini (19)
alikuwa akisoma Shule ya sekondari Maki na ameahidi kwamba akipata nafasi ya
kuendelea na masomo atasoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zake zilizoishia
njiani
“Natamani nami nipate nafasi ya
kuendelea na masomo, natamani nifike na chuo kikuu kama dada yangu.
Nilitamani nisome lakini kutokana na familia yangu kuwa duni niliishia njiani
japo dada yangu alijitahidi kunisomesha lakini ndiyo hivyo ameenda,” alisema
Yulia aliyeacha shule akiwa kidato cha tatu mwaka 2016.
Akwilina aliyekuwa mwanafunzi wa
mwaka wa kwanza NIT, alifariki dunia Februari 16 kwa kupigwa risasi wakati
polisi wakitawanya maandamano ya wafuasi wa Chadema waliokuwa wanaelekea
ofisi ya msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kinondoni kudai hati za viapo vya
mawakala wao
Wakati wa mazishi ya Akwilina
yaliyofanyika Februari 23, Olele wilayani Rombo, Kilimanjaro, waziri
Ndalichako aliahidi kumsomesha Angela (16) anayesoma kidato cha tatu katika
sekondari ya Kata ya Maki iliyopo tarafa ya Mashati wilayani Rombo hadi pale
atakapofikia kiwango cha elimu atakachoona kinafaa.
Profesa Ndalichako alisema
Akwilina alikuwa akitumia fedha zake za kujikimu kumsomesha mdogo wake, hivyo
kuanzia sasa yeye ndiye atakayetekeleza jukumu hilo na kuhakikisha binti huyo
anapata elimu bora.
Angela akizungumzia ahadi ya
waziri Ndalichako alisema ameipokea kwa furaha
“Dada alijitahidi kwa kadri
alivyoweza ili nisome lakini ndiyo hivyo Mungu kamchukua inaniuma, niliona
ndoto yangu ya elimu ndiyo imefika mwisho. Nikichukuliwa na waziri
nitapambana kwa kadri niwezavyo hadi nimpite hata dada yangu alipofikia,”
alisema Angela.
Alimzungumzia pia Yulia akisema,
“Nitafurahi kama waziri atamsaidia dada yangu aliyeacha shule akiwa kidato
cha tatu, dada yetu (Akwilina) alikuwa ni tegemeo letu,” alisema.
Kuanua tanga Shughuli ya kumaliza
msiba, itafanyika leo ili kuiwezesha familia kuendelea na mambo mengine.
Shirima alisema shughuli zote
zilizopangwa na Serikali katika msiba huo zilifanyika vizuri na kama kuna
changamoto zilizojitokeza ni ndogondogo.
|
|||
FAMILIA YA AKWELINA YAOMBA MSAADA KWA WAZIRI NDALICHAKO
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 26, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment