Rais Magufuli amwalika Mnangagwa



Rais John Magufuli amemkaribisha Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe kutembelea nchini.

Dk Magufuli ametoa mwaliko huo leo Alhamisi Januari 25,2018 alipoagana na Balozi wa Zimbabwe nchini anayemaliza muda wake Edzai Chimonyo.

“Naomba umwambie Rais Mnangagwa kuwa namkaribisha atembelee Tanzania na namtakia heri katika majukumu yake, natarajia ataendeleza uhusiano na ushirikiano wetu ili tuweze kujiimarisha zaidi kiuchumi kwa manufaa ya nchi hizi mbili,” amesema Rais Magufuli katika taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amempongeza Balozi Chimonyo kwa uwakilishi mzuri alioufanya kwa miaka 10 aliyoiwakilisha Zimbabwe nchini.

Pia, Dk Magufuli amemuomba Balozi Chimonyo kumfikishia pongezi Rais Mnangagwa kwa kuchaguliwa kuongoza Zimbabwe.

Amemhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kidugu uliopo kati yake na Zimbabwe.

Balozi Chimonyo ameshukuru Rais kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chake cha ubalozi nchini na amempongeza kwa namna anavyoiongoza nchi.

Ametaja baadhi ya mambo yanayofanywa kwa mafanikio kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa, ujenzi wa miundombinu na hasa barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Balozi Chimonyo aliyekuwa kiongozi wa mabalozi wa Afrika na kaimu kiongozi wa mabalozi wote wanaowakilisha nchi zao Tanzania amesema wanafurahishwa na wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli, ikiwemo kuhamia makao makuu Dodoma.

Rais Magufuli amwalika Mnangagwa Rais Magufuli amwalika Mnangagwa Reviewed by KUSAGANEWS on January 25, 2018 Rating: 5

No comments: