Polisi Arusha waanza Oparesheni ya Kukagua magari yanayobeba wanafunzi

JESHI la Polisi kikosi cha Usalama barabarani mkoa wa Arusha, kwa kushirikiana na chuo cha Ufundi cha Arusha,(ATC) kwa pamoja wameendesha zoezi la kukagua ubora wa magari ya kubebea wanafunzi na kubaini kuwa kati ya magari 60 yaliyokaguliwa   leo jumamosi ,24 yamegundulika kuwa na hitilafu na kung’olewa namba za usajiri.

Kamanda wa jeshi la Polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, amesema zoezi hilo la  ukaguzi wa magari hayo ni maalumu na kwamba Magari yenye hitilafu yanang’olewa  namba zake ili wamiliki wakayafanyie marekebishe ndipo yaruhusiwe kutumika tena.

 Amesema katika zoezi hilo lililofanyika  mapema leo katika chuo cha ufundi Arusha jumla ya magari 60 yamekaguliwa na miongoni mwa magari hayo 24 yamebainika kuwa na hitilafu na hivyo kung’olewa namba ili yakarebishwe na yakaguliwe tena ndipo yataruhusiwa.

Kamanda Mkumbo, amesema lengo la zoezi hilo sio kukwaza watoto na wazazi bali kuhakikisha magari yawe kwenye ubora  unaotakiwa wa kubeba wanafunzi.
Amesema zoezi hilo limeanza wiki hii na litafanyika tena wiki ijayo na kwamba ambao watakaokuwa wamekaidi zoezi hilo magari yao yatakamatwa na hayataruhusiwa kufanya kazi hiyo ya kubeba na kusafirisha wanafunzi.

Kamanda Mkumbo,amesema wameamua kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha ambacho kina wataalamu wengi wa magari waliobobea katika fani ya ufundi ili kusaidia ukaguzi wa magari hayo lengo ni kuepuka ajali.

Kamanda, Mkumbo,amesema baadhi ya wamiliki wanadhani magari yao yapo katika hali nzuri lakini kwenye zoezi hili yatagundulika ambayo yana hitilafu hivyo  wamiliki watapata muda wa kuyarekebisha.

Amesema mkoa wa Arusha umejipanga kuondoa ajali zinazosababishwa na magari ambayo yana hitilafu ambazo zimekuwa zikisababisha vifo na ulemavu kwa abiria.

Naye mkuu wa Idara ya Uhandisi  wa magari  wa Chuo cha Ufundi Arusha( ATC), Dkt Peter Mashingo,  ,amelipongeza jeshi la polisi kwa kutambua uwezo wa chuo hicho katika ukaguzi wa magari.

Amesema ukaguzi huo unahusisha mfumo mzima wa gari ambapo matatizo mengi yamegundulika kwenye mfumo wa Break,kutokuwa na mkanda na Injini za magari hayo.
,
Dkt. Mashingo,amesema serikali inapaswa kukitumia chuo hicho kwa kuwa kina  vifaa vingi vya kisasa vya ukaguzi wa magari na hivyo kukitumia chuo hicho kunapunguza gharama za ukaguzi wa magari.
Polisi Arusha waanza Oparesheni ya Kukagua magari yanayobeba wanafunzi Polisi Arusha waanza Oparesheni ya Kukagua magari yanayobeba wanafunzi Reviewed by KUSAGANEWS on January 27, 2018 Rating: 5

No comments: