Kiongozi wa chama cha Wiper Bw
Kalonzo Musyoka alipokabidhiwa uta na mshale na jamii ya Akamba mjini Machakos
Januari 19, 2018.
VIONGOZI
wa NASA wamewataka mabalozi wa mataifa ya Magharibi wakome kujihusisha na
masuala ya Kenya, wakishikilia kuwa ni lazima wataapisha vinara wao, Raila
Odinga na Kalonzo Musyoka.
Bw Musyoka, ambaye ni kinara wa
Wiper, alisema Kenya haihitaji usaidizi kutoka kwa mabalozi hao na akamtaka Balozi
wa Amerika, Robert Godec, akome kuingilia masuala ya nchi.
“Balozi wa Amerika kwanza anafaa
kuileta pamoja nchi yake ambayo sasa inachukuliwa kuwa imesambaratika.
Waamerika
wanaandamana kila siku kwa sababu hawana imani na uongozi. Watu kote
ulimwenguni wanalilia uhuru, ukweli na haki hali ambayo si tofauti hapa Kenya,”
akasema.
Alimtaja Bw Godec kuwa ndumakuwili
ambaye amekuwa akiegemea upande wa Jubilee huku akiwataka viongozi wa NASA wawe
na subira.
Bw Musyoka alisisitiza kuwa yeye na
Bw Odinga walishinda Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 2017 lakini wakaibiwa.
“Tulishinda uchaguzi huo peupe
lakini Mahakama ya Juu ilipoamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)
ifungue sava, Jubilee iliwatisha wakakataa kufungua. Kama wanaamini
hatujashinda, basi waagize sava zifunguliwe ili ulimwengu ujue ni nani msema
kweli,” akasema.
Wakizungumza wakati wa mkutano wa
Bunge la Wananchi katika bustani ya Uhuru, katikati mwa mji wa Mombasa, Bw
Odinga alisema viongozi wa Jubilee wanarudisha Wakenya siku za giza kwa kutaka
kuongoza wao na kubadilisha katiba.
Alimshambulia Bw Kenyatta kwa hatua
yake ya kuteua wakuu wa polisi akisema hiyo kinyume cha sheria.
“Wakenya wanafaa kuwakataa Uhuru na
Ruto na wapinge mipango yao ya kutaka kuturidisha siku za nyuma. Sisi tunaenda
Kanani nao wanataka kuturudisha Misri.”
Bw Odinga alisema NASA itafanya
mikutano Suswa eneo la Narok, Migori na Kisii kabla ya kuelekea Nairobi katika
sherehe ya kuapishwa kwake.
“Tuko na mwelekeo na safari hii ya
Kanani. Tunaelekea huko na mutasikia tarumbeta ikilia wakati tunafika. Nia yetu
inaendeshwa na Wakenya ndiposa tuko katika ziara hii,” akasema Bw Odinga.
Bw Kalonzo pia aliishambulia Jubilee
kwa kishindwa kutimiza ahadi zake, ikiwemo elimu ya bure ya sekondari.
“Waliiga mipango yetu ambayo ilikuwa
tumeipanga vilivyo na sasa wameshindwa kuitekeleza. Mmeona elimu ya bure
nyinyi?” akauliza.
Lakini akizungumza wakati wa ibada
katika Kanisa Katoliki la Magundu, Kaunti ya Tharaka-Nithi, Seneta Kithure
Kindiki aliwakosoa viongozi hao wa NASA kwa kuwapotosha wafuasi wao.
Alisema Katiba ya Kenya inaeleza
vyema jinsi mtu anavyoweza kuwa rais na kwamba mamlaka hayo hayawezi
kuchukuliwa kwa nguvu.
“Hata kama Bw Odinga na Bw Musyoka
watalishwa kiapo barabarani, wanajua vizuri kuwa hawana Ikulu wanakoweza
kwenda. Kiapo hicho hakina msingi wowote,” akasema.
NASA yawataka mabalozi wakome kuingilia siasa za Kenya
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 22, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment