Jaji Ramadhan ataka majaji kumuenzi Jaji Kisanga

Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani amemzungumzia Jaji Robert Kisanga kuwa mtu aliyebobea katika taaluma na hakuwahi kujihusisha na rushwa.

Amesema hayo leo Alhamisi Januari 25,2018 Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kuhani msiba wa Jaji Kisanga (85).

Jaji Ramadhani amesema hakuna hata siku moja aliwahi kusikia malalamiko dhidi ya Jaji Kisanga kutokana na uadilifu wake.

"Mimi ni miongoni kwa watu waliopitia kwenye mikono yake, yeye ndiye aliyenifundisha masuala ya Mahakama ya Rufaa," amesema.

Amesema, “Alikuwa mahiri kwenye kazi na kama uko naye kwenye kesi ni muhimu usome sana kwa sababu alikuwa anasoma na kila jambo alilichimba kwa undani."

Jaji Ramadhani amesema, "Naweza kusema ni miongoni mwa majaji waadilifu, kwake rushwa ilikuwa mwiko, hakuwahi kujihusisha na vitendo hivyo ndiyo sababu sikuwahi kusikia malalamiko dhidi yake."

Amesema majaji wanatakiwa kujifunza tabia hiyo kutoka kwa Jaji Kisanga.

"Majaji wanapaswa kutambua kuwa hakuna kitu kibaya kama kuuza utu wa mtu, mwenzetu Kisanga alizingatia mno sheria na hata mawakili waliokuwa wanapangiwa kesi kwake walikuwa wanajipanga," amesema.

Jaji Kisanga alifariki dunia Jumanne Januari 23,2018 katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya saratani.

    
Jaji Ramadhan ataka majaji kumuenzi Jaji Kisanga Jaji Ramadhan ataka majaji kumuenzi Jaji Kisanga Reviewed by KUSAGANEWS on January 25, 2018 Rating: 5

No comments: