Jaji Mkuu Profesa
Ibrahim Juma amewataka wananchi kuchukua hatua dhidi ya maofisa wa Mahakama
wanaokiuka maadili ya kazi na wanaojihusisha na vitendo vya rushwa badala ya
kulalamika.
Pia, ametaka wananchi
kutambua wanapokwenda mahakamani si lazima washinde ndipo waone haki
imetendeka kwa kuwa uamuzi wa Mahakama ni mchakato unaopitia mtiririko maalumu.
Profesa Juma amesema
hayo leo Jumapili Januari 28,2018 alipozindua Wiki ya Sheria katika viwanja vya
Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
“Mahakama inawathamini wananchi. Tumeweka matangazo kwenye ngazi
mbalimbali za Mahakama ambayo yanaonyesha namba za simu za wote wanaohusika,” amesema.
Profesa Juma amesema, “Kama mwananchi akiona hatendewi
haki labda anaombwa rushwa, badala ya kulalamika tu atumie namba zile za simu
kupiga kwa mamlaka husika, hasa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa) ambao ndio wanahusika na suala hilo.”
Alisema, “Mwananchi akiwa analalamika tu bila kuchukua
hatua hawezi kuisaidia Mahakama, kwa hiyo waanze kuchukua hatua.”
Amewataka watumishi wa
Mahakama na watoa haki kuwa na maadili mema na kutojihusisha na vitendo vya
rushwa ili wananchi wawe na imani na Mahakama.
Jaji mkuu amesema
kumekuwa na dhana kuwa mtu anapokwenda mahakamani ni lazima ashinde ndipo
anaona kuwa haki imetendeka.
Amesema ili haki
ipatikane kuna mlolongo wa hatua na utaratibu wa kufuata na la msingi ni mtu
kusikilizwa ndipo Mahakama inatoa uamuzi.
“Sasa maamuzi yanayotoka si lazima wewe ushinde, huo ndio msingi
wa haki. Wananchi wengi wanadhani kwamba wakienda mahakamani ni lazima tu
washinde,” amesema.
Share this:
Jaji Mkuu awataka wananchi kuchukua hatua dhidi ya maofisa wanaojihusisha na rushwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 28, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment