DC Kilwa akerwa na kiwango kidogo cha ufaulu, awakamia wazazi na walezi wazembe

Na. Ahmad Mmow.

MKUU wa wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai amewataka na wazazi na walezi wilayani humo wahakikishe watoto wao wanaripoti shuleni ndani ya muda ulilopangwa ili wasichukuliwe hatua kali za kisheria.

Ngubiagai ametoa agizo hilo leo wakati wa kikao cha kupanga mikakati ya kuinua kiwango cha elimu wilayani humo, kilichofanyika katika mamlaka ya mji mdogo wa Kilwa Masoko.

Amesema wazazi na walezi wilayani humo hawana budi kuwapeleka watoto wao waliochaguliwa kujiunga na shule za sekondari mwaka huu ndani ya muda uliopangwa. Akibainisha kwamba  watakaoshindwa kufanya hivyo watakutana na mkono wa sheria.

"Mimi kama msimamizi wa utekelezaji wa sera zilizotokana na ilani ya uchaguzi ya chama kilichounda serikali sipotayari kuona wananchi ninao waongoza hawathamini elimu. Ikifika tarehe 31 Machi, mwaka huu mzazi au mlezi ambae mtoto wake atakuwa hajariporiti shuleni, lazima ataniona mbaya, "alionya Ngubiagai.

Alisema ni jambo la aibu kuona wilaya hiyo imekuwa ya mwisho katika mkoa  wa Lindi wenye wilaya sita, na 160 miongoni mwa wilaya 186 za nchi hii katika ufaulu wa mitihani wa shule za msingi katika mwaka 2017.

Akioneshwa kukerwa na matokeo  hayo mabovu ya ufaulu, Ngubiagai alisema ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambacho kimeunda serikali imeweka sekta ya elimu kuwa ni kipaumbele chake cha kwanza. Hali inayosababisha serikali itenge na kutumia takribni shilingi 23 bilioni kila mwezi katika sekta hiyo.

Mbali na kuwaonya wazazi na walezi, mkuu huyo wa wilaya ya Kilwa aliwataka walimu, waratibu na maofisa elimu wakerwe na matokeo hayo na kuchukua hatua ambazo zitaonesha wanaweza kufanya mabadiliko na watabadilisha matokeo mwaka huu. 

" Ninyi ni viongozi, zingatieni sifa za kiongozi mzuri. Wote mnajua kwamba kiongozi safi anatakiwa kuwa muadilifu, mbunifu, mwenyeuthubutu, msikivu na mzalendo. Changamoto kubwa na sababu ya hali hii ni utoro na mimba. Tushirikiane kukomesha yote hayo, "alisema Ngubiagai.

Wilaya Kilwa yenye halmashauri moja na majimbo mawili ya uchaguzi ina shule za msingi 106, na shule za sekondari 27. Ikiwamo shule moja ya binafsi. Huku 26 zikiwa za serikali.
DC Kilwa akerwa na kiwango kidogo cha ufaulu, awakamia wazazi na walezi wazembe DC Kilwa akerwa na kiwango kidogo cha ufaulu, awakamia wazazi na walezi wazembe Reviewed by KUSAGANEWS on January 25, 2018 Rating: 5

No comments: