Siku tatu
baada ya Mkuu wa Wilaya ya Siha, Onesmo Buswelu kupanda jukwaani kumnadi
mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Siha, Dk Godwin Mollel, Chadema imesema
itamfikisha katika kamati ya maadili kama ilivyoshauriwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC).
Mkuu huyo wa
wilaya alipanda jukwaani Januari 21 katika uzinduzi wa kampeni za Dk Mollel
katika viwanja vya KKKT Karansi, huku akisema Serikali haijaribiwi hivyo ni
vyema kila mmoja akahakikisha anadumisha amani na kufanya siasa za kistaarabu
kipindi chote cha kampeni.
Baada ya kauli
yake hiyo, Mwananchi lilizungumza na mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Ramadhani
Kailima na kubainisha kuwa mkuu huyo wa wilaya hakufanya jambo sahihi.
Kailima
alisema vyama vinavyoshiriki uchaguzi katika jimbo hilo ndio vyenye jukumu la
kumshtaki katika kamati ya maadili inayoundwa na wajumbe wa vyama hivyo katika
jimbo husika na kwamba, jambo hilo linapaswa kufanyika ndani ya saa 72, tangu
apande jukwaani.
Akizungumzia
mchakato wa kumshtaki Buswelu, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya
nje wa Chadema, John Mrema alisema watawasilisha malalamiko yao yenye hoja
tano.
Kwa mujibu wa
Kailima, kama kuna uvunjifu wa maadili, kamati hiyo ina mamlaka ya kuwasilisha
hilo katika ngazi nyingine ya kisheria kama polisi au kwa mkurugenzi wa
mashtaka (DPP).
Uchaguzi wa
Siha na Kinondoni unaovihusisha vyama 12 utafanyika Februari 17, huku ukitajwa
kuwa ni mpambano mkali baina ya CCM na Chadema.
Uchaguzi huo
unafanyika baada ya waliokuwa wabunge; Mollel (Siha-Chadema) na Maulid Mtulia
(Kinondoni-CUF) kujivua uanachama wa vyama hivyo kwa maelezo kuwa wanamuunga
mkono Rais John Magufuli na baadaye kujiunga CCM.
CCM imempitisha
Mtulia kugombea Kinondoni na Mollel (Siha), huku Chadema ikimsimamisha naibu
katibu mkuu wake (Zanzibar), Salum Mwalimu (Kinondoni) na Elvis Mosi (Siha).
Chadema kumburuza DC kamati ya maadili
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment