Serikali ya Tanzania ijipange kuikabili njaa Makala ya General Ulimwengu



Mwaka huu tulioukaribisha hivi majuzi unaonekana kama wenye changamoto katika maeneo kadhaa, na matatizo hayo huenda yakashadidiwa na uhaba wa chakula unaoanza kujitokeza, anahoji Jenerali Ulimwengu.

Kupatikana (ama kutopatikana) kwa chakula cha kutosha katika nyingi ya nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara mara zote hutegemea wingi wa mvua na jinsi zilivyonyesha, na kwa mwaka uliopita mvua zimekuwa kidogo na zilizonyesha holela nchini kote.

Katika majira ya masika (mvua ndefu) ya mwaka 2016, maeneo mengi yalipata mvua nzito, baadhi zikiambatana na mafuriko, na athari ya mvua hizi ilikuwa ni kuharibu na kusomba mazao yasiyokomaa ikiwa hakuna tena wasaa kwa mkulima kupanda upya. Katika maeneo mengine mvua hazikutosha hata kidogo. Mvua za vuli (mvua fupi) zilikuwa haba zaidi.

Hali hii imeifanya Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Tanzania (TMA) kutoa hadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo uhaba wa chakula, ikieleza ukosekanaji wa mvua kama matokeo ya mabadiliko ya tabia-nchi ambayo yamesababisha ukame na kusababisha mito, maziwa na mabwawa kutojaa. Hii imekifanya kilimo cha umwagiliaji kisiwezekane.  

Mbunge maarufu wa kambi ya upinzani, Zitto Kabwe, ametoa mwito kuhusu anachokiona kama zahma inayoinyemelea Tanzania ya uhaba wa chakula, akiishauri serikali itangaze baa la njaa, huku akiieleza hali hiii kama matokeo ya mipangilio dhaifu ya serikali.

Akizungumza mwishoni mwa mwezi wa Disemba, Zitto alisema kwamba nchi ilikuwa imebakiwa na tani 90, 000 peke yake za nafaka, ambazo alisema zinaweza kulisha watu wenye mahitaji ya chakula kwa muda mfupi mno.

Serikali yakanusha 

Naye waziri anayeshughulikia kilimo, Charles Tizeba, hakuchelewa kumjibu Zitto, akisema hali haikuwa mbaya kama ilivyokuwa imedaiwa, ingawaje alikiri  kwamba maeneo machache yalikuwa yamepata matatizo kidogo ambayo serikali ilikuwa na uwezo wa kuyakabili.

Gazeti moja la kila siku lilionya dhidi ya hatari ya wanasiasa kugeuza tatizo la njaa kama kete za kushindaniwa katika malumbano ya kisiasa, likisema ni vyema serikali iyachukulie kwa umakini stahili maonyo inayopewa na viongozi wa upinzani.

“Tunaamini kwamba kauli za kisiasa (kuhusu njaa) hazitakuwa mtego wa kuficha ukweli kama kuna sehemu nchini wanataabika kwa njaa; ni imani yetu kwamba wanasiasa na viongozi wa serikali hawatalifanya suala la chakula kuwa kete ya kisiasa,” lilionya Mwananchi. 

Pia gazeti liliongeza kwamba ni busara kwa serikali “kuwaandaa wananchi kwa kwaelimisha (juu ya) umuhimu wa kuweka akiba ya chakula kitakachotosha kwa muda mrefu” ili kuondokana na tatizo hili miaka nenda miaka rudi.

Changamoto kwa utawala wa Rais Magufuli

Hata hivyo, kutakuwapo na tatizo kuhusu jinsi serikali itakavyokabiliana na tatizo hili muhimu. Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza hivi karibuni kwamba serikali yake haiko tayari kugawa chakula cha bure kwa wenye njaa, kwani hiyo si kazi ya serikali. Itabidi kuangalia kwa makini nini serikali itafanya pale kisu kikakapogusa mfupa, wakti watu wanaanza kufa kwa njaa.

Yamekuwapo malalamiko kuhusu upungufu wa fedha katika mzunguko wa uchumi. Baadhi ya biashara zimefilisika na baadhi zimepunguza sana shughuli za uzalishaji kutokana na hatua za kubana matumizi zinazotekelezwa tangu Magufuli aingie madarakani mwaka 2015 akinadi dhamira yake ya kupambana na ufisadi, ubadhirifu serikalini na ukwepaji wa kodi.

Wakati huo huo, serikali imekuwa ikishindwa kuwalipa wakandarasi binafsi na watoa huduma kwa serikali, na hii imekuwa na maana kwamba waajiri hawawalipi kwa muda unaotakikana wafanyakazi wao. Katika kipindi hiki cha kufungua shule, wazazi wengi watakuwa na machungu ya kuwapeleka watoto shule wakati wao hawajapata stahili yao makazini.

Wala hali haionekani kuwa itabadilika hivi karibuni. Zipo dalili kwamba nchi wafadhili wataendelea kupunguza misaada kwa serikali ya Tanzania kusaidia bajeti ya serikali kwa sababu nchi hizo zimekuwa zikieleza kutoridhishwa kwake na utendaji wa serikali hiyo katika nyanja za utawala bora, haki za binadamu na uhuru wa habari.

Ni wazi kwamba Tanzania inategemea sana uungwaji mkono wa wahisani kwa bajeti yake, na iwapo utaendelea kupungua, kutakuwapo na matatizo, hususan sasa ambapo inaelekea yataongezeka kutokana na tishio la njaa.  
Mwandishi: Jenerali Ulimwengu
Mhariri: Mohammed Khelef   

Serikali ya Tanzania ijipange kuikabili njaa Makala ya General Ulimwengu Serikali ya Tanzania ijipange kuikabili njaa Makala  ya General Ulimwengu Reviewed by KUSAGANEWS on January 14, 2017 Rating: 5

No comments: