POSHO ZA MWENGE KUJENGA MADARASA MALINYI



MKUU wa Wilaya ya Malinyi mkoa wa Morogoro, Majura Kasika ameagiza posho iliyookolewa kutokana na kufutwa kwa safari ya maofisa watatu na madereva wawili wa wilaya hiyo kwenda kwenye kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka huu mkoani Simiyu, kuelekezwa katika kuongezea nguvu ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu sita ya vyoo.

Hatua ya viongozi hao kufuta safari hiyo, ilitokana na agizo la Rais John Magufuli aliyeagiza viongozi kutoka mikoa yote nchini, nje ya Simiyu, kutokwenda katika maadhimisho hayo na wale ambao walikuwa tayari wamechukua posho kuzirejesha mara moja.

Kasika alisema jana kuwa kutokana na agizo hilo la Rais, wilaya ya Ulanga iliweza kuokoa Sh 2, 580,000 ambazo sasa zitaelekezwa katika kuchangia ujenzi huo wa vyumba viwili vya madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi ya Kitongoji cha Lumbanga Kijiji cha Misegesege Kata ya Malinyi.

Akizungumza na wananchi wa kitongoji hicho cha Lumbanga, wakati akiendesha kazi ya uhamasishaji wa uchangiaji wa michango ya maendeleo kwa ajili ya kupata fedha za kuanza kufyatua matofali ya ujenzi huo, Mkuu huyo wa wilaya alisema fedha hizo zitaelekezwa mara moja katika mradi huo.

Uamuzi huo wa Mkuu wa Wilaya, uliungwa mkono na Mbunge wa Malinyi, Dk Haji Mponda ambaye aliahidi kuchangia Sh 500,000 katika mpango huo, huku wananchi wakiahidi kuchangia Sh 30,000 kwa kila kaya.

 

POSHO ZA MWENGE KUJENGA MADARASA MALINYI POSHO ZA MWENGE KUJENGA MADARASA MALINYI Reviewed by KUSAGANEWS on October 21, 2016 Rating: 5

No comments: