Serikali imesema ujangili ni janga la taifa linalohitaji kila mtu
aguswe moyo wake ili ashiriki katika kulitokomeza na kwamba itafanya
kila linalowezekana kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuimarisha mifumo
ya uhifadhi.
Waziri wa maliasili na utalii Mhe.Lazaro Nyalandu ameyasema hayo
jijini Dar es Salaam wakati akizindua kampeni mpya ya kupambana na
ujangili, itakayotekelezwa kwa kushirikiana na asasi za kimataifa za
Wildaid na African Wildlife Foundation, pamoja na mabalozi wapya wa
kampeni hiyo mwanamuziki Ali Kiba na Jacquiline Mengi ambapo amesema
wizara yake itahakikisha vijana wanakuwa sehemu ya ulinzi wa rasilimali
hiyo.
Wakizungumza katika uzinduzi huo uliohudhuriwa na watu mashuhuri
akiwemo mabalozi wa Marekani na China, balozi wa mpango huo mwanamuziki
Ali Kiba na miss Tanzania wa mwaka 2000 Jacquiline Mengi wamewahamasisha
watanzania kushiriki kikamilifu katika kudhibiti ujangili ili
kuwanusuru Tembo, na wanyama wengine walio katika hatari ya kuangamizwa.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa dini waliohudhuria uzinduzi
huo wamesema kuua wanyama kwa njia zisizostahili haikubaliki popote,
kwani wanyama pia wana haki zao za kuishi na kuitaka serikali kuwa na
mkakati wa muda mrefu ambao ni kuinua kizazi kitakachopenda wanyama na
kuchukia ujangili.
Naye afisa mtendaji mkuu wa asasi ya Wildaid Bw. Peter Knights
amesema kampeni ya kutokomeza ujangili itafanikiwa duniani iwapo nguvu
kubwa itatumika kuwashughulikia wafanyabiashara haramu wa kati badala ya
kushughulika na wanavijiji peke yake na kuongeza kuwa utafiti
umeonyesha kuwa tanzania imepoteza tembo kwa asilimia 60.
Mabalozi waunganisha nguvu na wasanii wa Tanzania kupiga vita ujangili.
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 18, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment