Ndiyo ligi ambazo hata klabu zimekuwa na mapato
makubwa na wadhamini wengi jambo ambalo limekuwa likiwanufaisha mpaka
wachezaji wa ndani na wale wa kigeni kwenye ligi hizo.
Ligi za DR Congo, Sudan, Tunisia, Mali, Morocco,
Nigeria, Ghana, Angola, Zimbabwe na Ivory Coast zinatajwa kama Ligi
ngumu na lakini inaelezwa kwamba klabu nyingi kwenye nchi hizo hazilipi
vizuri kutokana na kuyumba kiuchumi.
Tukio linalozungumzwa na wadau wengi kwa sasa ni
lile la Simon Msuva wa Yanga kutorokea Afrika Kusini kufanya majaribio
kwenye klabu ya Bidvest Wits bila idhini ya klabu. Mchezaji huyo
alifanya majaribio kwa siku kadhaa na sasa anasubiri majibu ingawa
taarifa za awali zinadai kwamba amefuzu.
Kikanuni Wits wamefanya makosa kumfanyia majaribio
Msuva bila ya kupata idhini ya maandishi kutoka Yanga. Kocha wa Yanga,
Hans Pluijm anasema Msuva alimuomba ruhusa lakini uongozi unakana kwamba
haukuwa na taarifa na umeanza mchakato wa kuishtaki Wits.
Lakini ukiangalia rekodi za miaka ya hivi
karibuni, kumekuwa na utata pale mchezaji wa Yanga anapotaka kwenda
kufanya majaribio au anapopata timu nje, Yanga wamekuwa wagumu kumuachia
mchezaji kuondoka ndio maana baadhi yao wamekuwa wakifanya uamuzi wa
kutoroka kama alivyofanya Msuva.
Hatuungi mkono alichofanya Msuva lakini ukiangalia
Ivo Mapunda wakati yuko Yanga alitokewa na hali kama hiyo akaamua
kutorokea St.Georges baadaye Jerry Tegete akapata dili naye akabaniwa
ikayeyuka. Maoni yetu ni kwamba Msuva amefanya kosa lakini Yanga wakae
chini wajadiliane jinsi ya kutatua hilo tatizo kwa masilahi ya klabu,
mchezaji mwenyewe na Taifa kwa ujumla.
Mchezaji huyo kwa sasa yupo kwenye fomu na ndio
wakati wake wakufanya mambo makubwa, Wits wakileta dau Yanga wajadiliane
kiungwana wamuachie akatafute maisha Afrika Kusini.
Akienda kucheza kule timu ya Taifa itanufaika
zaidi na huenda ndani ya kipindi kifupi akauzwa kwenye Ligi kubwa zaidi
katika Mabara mengine. Mrisho Ngassa akifanya vizuri na Free na Msuva
naye akiwa fiti itatusaidia kuongeza nguvu kwenye timu ya Taifa kwavile
Afrika Kusini klabu zina mashindano mengi, hali ambayo inamuweka
mchezaji kwenye hali nzuri zaidi tofauti na Tanzania kwenye Ligi moja
tu.
Yanga isitamke dau la kukomoa au kukatisha tamaa,
itumie uungwana ili kuokoa kipaji cha Msuva kwa vile nafasi zenyewe kwa
mchezaji kuzipata kama hizo ni adimu na akienda akifanya vizuri
anafungua njia pia kwa wengine kuiangalia ligi ya Tanzania.
Halafu ifike mahali klabu zetu na zenyewe
zibadilike, zijenge mazingira ya urafiki na klabu nyingine za Afrika na
Dunia na zijivunie kufanya biashara ya wachezaji pamoja na kubadilishana
wataalamu kwavile dunia imekuwa kijiji na hakuna kisichowezekana.
Yanga itumie uungwana kumsaidia Msuva
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 13, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment