BADO MAMBO MAGUMU POLISI

Wakati mjadala wa kifo cha ofisa wa polisi anayedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu ukipamba moto, mawakili na maofisa wa zamani wa Jeshi la Polisi wametofautiana juu ya uwezekano wa mtu kujinyonga mahabusu.

Tukio hilo, licha ya kukumbushia matukio mengine ya mahabusu kudaiwa kujinyoga wakiwa mikononi mwa polisi, limeibua maswali saba yanayolifanya liwe tukio lenye utata na kitendawili kinachohitaji kuteguliwa.

Licha ya mawakili na maofisa hao wa zamani kufunguka, madaktari nao wametofautisha kifo kitokanacho na mtu kujinyonga mwenyewe au kunyongwa na mtu mwingine halafu ionekane amejinyonga ili kupoteza ushahidi fulani au sababu nyingine.

Grayson Mahembe (26), mkaguzi msaidizi wa polisi anadaiwa kukutwa amejinyonga katika mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi mjini Mtwara asubuhi ya Januari 22, wakati yeye na maofisa wengine saba walipokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za mauaji.

Maofisa hao wanatuhumiwa kumuua kwa makusudi mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi na kuutupa mwili wake huko Kijiji cha Hiari wilayani Mtwara ili asifuatilie fedha walizompora. Mauaji hayo yanasadikika yalifanywa Januari 5, baada ya askari hao kuchukua Sh70 milioni kutoka kwa mfanyabiashara huyo.

Tayari maofisa saba waliokuwa wakishikiliwa wamefikishwa mahakamani juzi mchana kwa tuhuma za kuua kwa kukusudia.

Akizungumzia msiba wa mwanaye, mama mzazi Hawa Ally alisema bado hawajakabidhiwa mwili kwa ajili ya mazishi kwani wameambiwa uchunguzi bado unaendelea na watatoa heshima zao za mwisho pindi jeshi litakapokamilisha utaratibu wa kukusanya ushahidi kwa ajili ya mashtaka yaliyopo mahakamani.

Wakati taarifa ya Polisi Mkoa wa Mtwara ikieleza alijinyonga akiwa mahabusu, baadhi ya wananchi wanahoji ilikuwaje akajinyonga bila watuhumiwa wenzake kuona au kusikia purukushani.

Tayari ndugu, akiwamo baba mzazi wa marehemu, Gaitan Mahembe wamelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza kiini cha kifo hicho, wakidai mazingira ya kujinyonga kwake hayawaingii akilini.

 

Polisi wastaafu wafunguka

Ofisa wa Polisi aliyestaafu akiwa na cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Yusuph Mruma alisema mtuhumiwa kujiua akiwa mahabusu ni jambo linalowezekana kutegemea mazingira ya mahabusu aliyomo.

“Hata shati mtu anaweza kujinyongea. Unataka kuniambia mtu hawezi kujinyonga kwa suruali? Kama mazingira ya lockup (mahabusu) yanaruhusu kujining’iniza si jambo la kushangaza kujinyonga,” alisema.

“Lakini hii itatokea tu kama yuko mwenyewe mahabusu. Kama kuna watuhumiwa wengine watapaza sauti na CRO atakuja. Haya ya kujinyonga mahabusu mara nyingi ni kama yuko mwenyewe,” alisema Mruma.

Wakili Hudson Ndusyepo, aliyewahi kuwa kachero wa polisi, mwendesha mashitaka na sasa wakili wa kujitegemea, alisema mahabusi kujinyonga akiwa mahabusu ni jambo linalowezekana kutegemea mazingira.

“Hili linawezekana kwa sababu ni binadamu, ana mbinu nyingi ikichangiwa na mazingira atakayokuwepo. Ni angalizo, kabla ya kuingia mahabusu sharti uvue mkanda na usiingie na kitu kinachoweza kutumika kuleta madhara,” alisema.

 

Maswali magumu

Wakizungumzia uwezekano wa mtu kujinyonga akiwa mahabusu, baadhi ya wanasheria, akiwamo Wakili Peter Madeleka walisema ni jambo lisilowezekana. “Kwa mazingira ya mahabusu za polisi, kujinyonga ni ngumu sana kwa sababu kabla hujaingia utatakiwa kuvua viatu, mkanda na utakabidhi mali kama fedha na simu ndipo utaingia,” alisema Madeleka.

Naye Tito Magoti, mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) alisema siyo rahisi kujinyonga ndani ya kituo cha polisi.

“Isitoshe, kama kuna watu ndani, itawezekanaje wakuone unajinyonga wakuachie?” alihoji Magoti.

 

Kinachotokea ukijinyonga

Wakati mjadala ukiendelea nchini kuhusu mahabusu za polisi kuwa na mazingira yanayomwezesha mahabusi kujinyonga hadi kufa, madaktari wameeleza kinachotokea mtu anapojinyonga au kunyongwa.

Dk Kareem Segumba ambaye ni mkuu wa Chuo cha St John cha Sayansi Shirikishi cha Jijini Mbeya, anasema kinachosababisha mtu aliyenyongwa au kujinyoga afe ni kuathiriwa kwa mzunguko wa damu mwilini.

“Tunapoongelea kujinyonga au strangulation kama tunavyoita kitaalamu ni ile hali ambayo mtu anajiua kwa makusudi au kundi la watu wanamuua kwa makusudi kutaka kitu fulani au kupoteza ushahidi,” alisema na kuongeza:

“Mara nyingi watu wanaojiua wenyewe huwa wanajining’iniza kwenye kitanzi. Sababu inayofanya afe ni kwamba mishipa mikubwa inayosambaza damu kutoka kwenye moyo inapita kushoto na kulia mwa shingo. Akijinyonga au kunyongwa, kile kitanzi kinakwenda kuikandamiza mishipa ya damu kuzuia usambazaji damu kwenda mwilini.”

Kwa maana hiyo, anasema mapafu yatajaa, damu itakuwa haifiki kwenye ubongo na moyo utasimama kufanya kazi kwa maana hauwezi tena kufanya kazi. Hili halitokei kwa anayekufa kwa kitanzi tu, hata akikabwa shingo kwa namna yoyote anaweza kupoteza maisha iwapo mkabaji atakandamiza hiyo mishipa.

“Hata ukimpiga mtu kabali kwa muda fulani, atakufa kwa sababu damu itakuwa haifiki kwenye moyo, ubongo wala mapafu. Ndiyo maana ili kuthibitisha mgonjwa amejinyonga au amenyongwa, utaona kuna michubuko kwenye shingo halafu ulimi umevimba na mapafu yamejaa. Tunaangalia hayo tunapofanya postmoterm,” alisisitiza Dk Kareem.

Kwa upande wake, Dk Issa Mmbaga aliyestaafu Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi na St Joseph anasema kujinyonga kunahusisha hewa ya oksijeni kutofika kwenye ubongo na moyo.

Kwa mujibu wa Dk Issa, hii inatokana na kukandamizwa kwa mshipa unaopeleka damu kichwani, hivyo kusababisha ubongo kufa.

 

Jeshi kuchunguza

Jeshi la Polisi limewataka wananchi wenye ushahidi wa mauaji na unyang’anyi wa fedha za Hamis kuuwasilisha kusaidia uchunguzi unaofanywa na timu ya makachero wakiongozwa na Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya Jinai, Camilius Wambura ambaye yuko mkoani Mtwara kwa siku kadhaa sasa.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa mwananchi endapo kuna mwenye ushahidi mwingine wa ziada wenye kuthibitisha uhalifu mwingine wa wahalifu hao, wawasilishe ushahidi huo kwa timu hiyo,” ilinukuu sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime.

Jeshi la Polisi limesema limeunda timu kuchunguza tukio hilo kwa kukusanya ushahidi utakaowezesha kuthibitisha tuhuma zinazowakabili askari wake.

“Yanayodaiwa kufanywa na maofisa na askari hao si maelekezo ya Jeshi la Polisi, bali ni matendo yao binafsi na tamaa za kutaka kujipatia fedha kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi,” imesema taarifa hiyo ya Misime.

 

BADO MAMBO MAGUMU POLISI BADO MAMBO MAGUMU POLISI Reviewed by KUSAGANEWS on January 28, 2022 Rating: 5

No comments: