Tembo wa Mkomazi waua watu wawili


Wakazi wawili wa vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, wamefariki dunia baada ya kushambuliwa na tembo waliovuka mipaka ya hifadhi na kuingia vijijini kwao

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe ni kwamba wanavijiji hao waliuawa juzi Jumapili saa 1.10 asubuhi katika vijiji viliyopo kata za Kizara na Kalalani wilayani hapa

Waliouawa ni Jumaa Kanju (24) mkazi wa kijiji cha Bombo Majimoto, kata ya Kizara na Habiba Ramadhani (70) mkazi wa Mtoni Bombo kata ya Kalalani ambao wote waliuawa wakiwa shambani.

Diwani wa Kata ya Mashewa, Seif Hillary amesema mauaji hayo yamewashtua wakazi wa vijiji hivyo kwa sababu mara nyingi tembo hufanya uharibifu wa mazao kwenye mashamba lakini haijawahi kutokea wakawashambulia binadamu

“Hili ni tukio la kwanza kwenye maeneo yetu haya kwa tembo kutoka Mkomazi kuwaua watu, tumezoea wakivamia mashamba na kuharibu mazao, tunaomba Serikali iangalie namna ya kufanya ili kunusuru maisha ya wananchi,”amesema Seif

Mkuu  wa  Askari  wa  Hifadhi  ya Taifa  Mkomazi, Laurent  Kawau amesema  kuwa baada  ya  kupata  taarifa  kutoka  kwa  viongozi  wa Kata  ya  Mashewa  waliweka  kikosi cha askari waliokwenda kuwaswaga tembo waliovuka mpaka na kwenda vijiji hivyo jirani.

“Mpaka sasa tumefanikiwa  kuwaswaga  tembo  hao kurudi  katika hifadhi yetu ya Mkomazi na wengine wameelekea katika msitu  wa Mashewa uliopo mbali na makazi ya wanakijiji,” amesema Kawau

Mkuu huyo wa ulinzi wa Mkoamazi aliwataka  wananchi  wa maeneo hayo kuchukua tahadhari kwa kuacha kutembea usiku pamoja na asubuhi na akatahadharisha kuacha kupiga kelele walipo wanyama hao kwani hao wakisikia kelele huzifuata sauti zilipo

Tembo wa Mkomazi waua watu wawili Tembo wa Mkomazi waua watu wawili Reviewed by KUSAGANEWS on August 21, 2018 Rating: 5

No comments: