Kasi ya Kangi haina kikomo na haitabiriki.


Wakati watu wakisubiri kuona spidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mh. Kangi Lugola itakapokwamia, kiongozi huyo ameonesha kutotabirika kutokana na vitendo vyake vinavyotokea kila siku ndani ya utendaji wake wa kazi. 

Spidi ya Waziri Lugola, inazidi kwenda mbele zaidi, baada ya tukio la leo la kumwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kumuweka rumande Askari Polisi aliyeshindwa kujibu swali lake lililohoji, "ni vitabu gani muhimu vinastahili kuwekwa katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa msaada wa huduma kwa raia"?

Lugola ametoa agizo hilo leo alipokuwa Arusha katika ziara yake ya kikazi ambayo ilikuwa ikihusisha kukutana na wadau wa utalii pamoja na kujadili mambo ya usalama na ajira kwenye sekta hiyo.

Hata hivyo baada ya agizo lake kuchukuliwa hatua Waziri Lugola alimtaka RPC kumtoa rumande askari huyo kwa kuwa amegundua kwamba askari huyo anakosa uelewa wa masuala ya utalii pamoja na diplomasia.           
             
Tukio la Waziri Lugola la kumuweka na kumtoa rumande askari polisi linakuja ikiwa siku chache tuu kupita tangu kutoa tamko la kutafutwa kwa mbwa kisha kusitisha tamko hili na kuzuia jamii ya kitanzania hususani waandishi wa habari kuacha kufuatilia tukio la kupotea mbwa wa Jeshi la Polisi anayejulikana kwa jina la Hobby, kwa kuwa jambo hilo kwa sasa lipo chini ya uchunguzi.

Julai 19, 2018, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alibaini upotevu wa mbwa huyo wakati alipokuwa kwenye ziara yake katika Kikosi cha Farasi na Mbwa kilichopo eneo la Bandari Jijini Dar es Salaam na kumuagiza IGP Sirro kutoa maelezo ya upotevu wa mbwa.

Pamoja na hayo, Waziri Lugola ameshamtaka IGP Simon Sirro amtafute mmiliki wa kampuni ya Lugumi popote pale alipo na kumfikisha ofisini kwake Julai 31 saa mbili asubuhi ili ajue hatma yake ikiwa ile ya kudaiwa kuwepo na ufisadi.

Sakata la Lugumi liliibuka bungeni kwa kile kilichodaiwa kuwa zipo dalili za ufisadi, kutokana na Sh. bilioni 34 zilizolipwa kwa kampuni ya Lugumi iliyopewa tenda ya kufunga vifaa vya kielektroniki vya kutambua alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchini ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeshindwa kukamilishwa..

Mbali na hilo Waziri Lugola pia amemuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) afike ofisini kwake Julai 25 akiwa na waliopewa tenda ya kuleta mtambo wa kutengeneza vitambulisho vya taifa ili kwenda kumueleza kwani mtambo huo haujaletwa au waende na pesa walizopewa na Serikali.

Waziri Lugola tayari ameshatoa matamko mengi na sasa ikiwa ni wiki ya tatu tangu alipoapishwa, kwa mujibu wake amesema anajitahidi kufanyia kazi maagizo yote aliyopatiwa wakati anaapishwa na kama Waziri ni wajibu wake kutafuta matokeo chanya ya haraka ili Rais aweze kupumzika na kuwatumikia wananchi kwenye maendeleo
Kasi ya Kangi haina kikomo na haitabiriki. Kasi ya Kangi haina kikomo na haitabiriki. Reviewed by KUSAGANEWS on July 23, 2018 Rating: 5

No comments: