Serikali imeonyesha dhamira yake ya dhati ya
kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo wa kuzalisha umeme baada ya kutenga Sh700
bilioni kwa ajili ya mradi wa Stiegler’s Gorge, kwa mujibu wa bajeti ya Wizara
ya Nishati iliyowasilishwa bungeni jana
Mradi huo, uliopewa jina la mgunduzi wa
Uswisi aliyefia eneo hilo mwaka 1907 baada ya kushambuliwa na tembo, utajengwa
katika Mto Rufiji, ndani ya Hifadhi ya Selous na unatarajiwa kuzalisha Megawati
2,100 za umeme
Akiwasilisha bajeti hiyo jana, Waziri wa
Nishati, Dk Medrad Kalemani aliomba chombo hicho cha kutunga sheria kiidhinishe
Sh1.69 trilioni kwa mwaka 2018/19, huku zaidi ya asilimia 40 zikitengwa kwa
mradi huo unaotarajiwa kuanza Julai
Dk Kalemani alisema mkandarasi atafanya kazi
za awali kwa miezi mitatu kabla ya kuanza ujenzi wa miundombinu ya mradi
unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 36
“Fedha za maendeleo za ndani Sh700 bilioni
zimetengwa katika mwaka wa fedha 2018/19 kwa ajili ya kuanza kutekeleza kazi
hizo,” alisema
Alizitaja kazi hizo kuwa ni ujenzi wa kambi
na ofisi za wafanyakazi na njia kuu za kupitisha maji
Dk Kalemani alisema katika mwaka wa fedha
2017/18, kazi iliyofanyika ni uchambuzi wa zabuni zilizowasilishwa na
makandarasi walioonyesha nia ya kutekeleza mradi huo
“Ujenzi wa njia ya msongo wa KV 33 kutoka
Dakawa kwa ajili ya kupeleka umeme utakaotumiwa na mkandarasi wakati wa ujenzi
wa mradi ulianza Novemba mwaka jana na unatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu,”
alisema
Mradi huo unatarajiwa kujengwa kwenye eneo
la kilomita 1,350 za mraba na litajengwa bwawa lenye urefu wa mita 134
Kwa mujibu wa mpango mkuu wa mfumo wa
nishati wa mwaka 2016, mahitaji ya umeme kwa ajili ya viwanda na shughuli za
biashara yataongezeka hadi asilimia 18 kati ya mwaka 2015 na 2020 kutokana na
maendeleo ya gesi, ujenzi wa miundombinu ya usafiri, kuongezeka kwa uwekezaji
kutoka nje, kukua kwa kiwango cha elimu na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano
Katika mpango huo wa mwaka 2016, haja ya
kuongeza uzalishaji umeme inaonekana kubwa kutokana na matumizi ya mkaa kufikia
asilimia 80 na hivyo mikakati ya umeme kutarajiwa kupunguza matumizi hadi
asilimia 49 ifikapo mwaka 2040
Hata hivyo, baadhi ya wabunge wamekuwa
wakipinga kuanza kutekelezwa kwa mradi huo wakitaka kwanza ufanyike upembuzi
yakinifu wa athari za kimazingira kabla ya utekelezaji kuanza, jambo ambalo
Serikali imesema linafanyika na sasa timu yake imeenda eneo hilo kuzungumza na
wadau
Pia wanaharakati za mazingira wanadai kuwa
utekelezaji wa mradi huo utaondoa hali ya uasilia wa eneo hilo na kusababisha
viumbe, mimea na wananchi kuhamishwa kupisha mradi pamoja na kuathiri shughuli
nyingine za kiuchumi kama utalii
Lakini jana, Dk Kalemani
alieleza umuhimu wa mradi huo mkubwa wa kuzalisha umeme akisema miongozi
manufaa ya Stiegler’s Gorge ni kuvutia watalii, hivyo kuongeza fedha za kigeni,
kuongezeka kwa shughuli za majini kama vile michezo ya majini
Alisema visima 10 ndani ya bwawa vitaongeza
mazalia ya samaki, mamba na viboko, hivyo kuvutia watalii
Waziri alisema litajengwa tuta la kuzuia
maji lenye urefu wa sawa na ghorofa 45 kwenda juu na upana wa kilomita moja
litakalovutia utalii na hata kutumiwa na maharusi walio fungate
Alisema manufaa mengine ni pamoja na kutunza
maji katika bwawa la mradi yanayoweza kumwagilia hekta 250,000 za mashamba,
hivyo kukuza shughuli za umwagiliaji.
Alisema bwawa hilo litakuwa na ukubwa wa
mita za mraba 914
Pia, kutoa huduma za kijamii katika maeneo
ambayo yanazunguka mradi huo ikiwamo wananchi hao kuruhusiwa kufanya uvuvi
Dk Kalemani alisema umeme utasambazwa maeneo
ya vijiji 49 vya jirani kutoka wilaya za Morogoro Vijijini, Kibiti, Rufiji,
Ulanga, Malinyi na Mlimba
Alisema wananchi hawataondolewa wala
kuhamishwa katika makazi yao na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (Dawasa)
imeshaanza kufanya utafiti wa mahali watakapochukua maji kwa ajili ya matumizi
ya majumbani kwa wananchi wa Pwani na Dar es Salaam
Katika mikoa hiyo, alisema maji yatapita
katika vijiji vya wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Temeke na Kigamboni,
hivyo kuingia katika mfumo wa maji wa Jiji la Dar es Salaam na kutoa ajira kwa
watu 10,000
Dk Kalemani alisema huo mradi utatoa huduma
za kijamii kwa kuchangia katika ujenzi wa shule, vituo vya afya na viwanja vya
michezo katika kaya zitakaozunguka mradi na wilaya za Malinyi, Ulanga, Morogoro
Vijijini, Kibiti, Rufiji, Mlimba na maeneo mengine ya jirani
Alisema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)
hutoa takriban Sh150 bilioni kwa mwaka kati ya hizo Sh66 bilioni huelekezwa
kwenye huduma za jamii katika miradi ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji
Dk Kalemani alisema mradi utakapokamilika
utazalisha Megawati 2,100. Alisema umeme utakaouzwa kwa wateja utaingiza Sh1.6
trilioni kwa mwaka.
Alisema kulingana na usanifu, mradi
unatarajiwa kudumu kwa miaka 80 tangu utakapoanza uzalishaji na kwamba, miradi
mingine ya Kihansi na Mtera, uhai wake ni angalau miaka 50
Kuhusu mpango wa kutunza mazingira, Dk
Kalemani alisema Tanesco itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya uendelezaji
mazingira kutokana na athari zinazoweza kujitokeza
Uagizaji wa mafuta
Katika hotuba yake, Dk Kalemani pia
alizungumzia Bandari ya Mtwara kuanza kupokea mafuta mwezi Juni kwa kutumia
mfumo wa uagizaji kwa pamoja
“Utaratibu wa kupanga bei ya mafuta
yatakayoingizwa kupitia bandari hiyo utazingatia utaratibu unaotumika katika
Bandari ya Tanga,” alisema
Alisema miundombinu ya kuhifadhia mafuta
iliyopo Tanga ina uwezo wa kutunza lita 26 milioni zinazotosheleza mahitaji ya
ukanda huo kwa sasa
Kuhusu usambazaji wa gesi asilia, alisema
katika mwaka wa fedha 2018/19, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
litaweka miundombinu itakayowezesha zaidi ya nyumba 2,000 kuunganishiwa gesi
asilia na kuisambaza katika mgahawa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na
kampuni ya usimamizi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam (Udart) na
kwa utekelezaji zimetengwa Sh20.9 bilioni
Alisema mradi wa bomba la kusafirishia
mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Uganda hadi Tanzania,
umetengewa Sh54.2 bilioni, fedha za ndani kwa ajili ya kukamilisha majadiliano,
usanifu wa kina wa kihandisi na kuwalipa wananchi watakaopisha mradi hu
Alisema mradi huo utakaogharimu Sh8.07
trilioni hadi kukamilika ujenzi, unatarajiwa kuanza Juni na kukamilika mwaka
2020.
Mradi wa umeme wa Stiegler sasa rasmi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment