Kesi ya kina Mbowe yanguruma mpaka saa mbili usiku Kisutu

Ubishani wa kisheria katika kesi inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake wanane uliilazimisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufanya kazi mpaka saa 1:58 usiku kabla ya kuahirishwa hadi Juni 11

Kiini cha ubishani katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa saa nane mchana jana ni upande wa utetezi katika kesi hiyo kuwasilisha pingamizi nane ukiomba mashtaka yanayowakabili washtakiwa yafutwe kwa sababu yana upungufu kisheria

Wakili wa utetezi Peter Kibatala katika ombi mbadala aliomba iwapo Mahakama itashindwa kuifuta hati nzima ya mashtaka, basi iyafute ambayo yana upungufu kisheria

Amedai maelezo kwa shtaka la nne, tano, sita na la saba yanawachanganya washtakiwa na hawawezi kujitetea kikamilifu

Pia, mashtaka hayo amedai ili kufunguliwa kunahitaji ridhaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambayo haipo

Wakili Kibatala aliwasilisha pingamizi hizo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi kuiambia Mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na walikuwa tayari kwa kufanya hivyo

Nchimbi baada ya kueleza hayo, Kibatala alisema ni kweli lakini wamewasilisha pingamizi hizo za kisheria

Kibatala alidai panapokuwa na pingamizi kwa mujibu wa sheria ni lazima lisikilizwe kwanza. Upande wa mashtaka haukupinga na mahakama iliridhia
Kibatala alidai kibali kilichotolewa na DPP kuipa ridhaa Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo kina upungufu kwa sababu hakisemi kimetolewa kwa mashtaka yapi na kwamba kimetaja majina ya washtakiwa bila kufafanua makosa waliyotenda.

 “Siyo kazi ya Mahakama kutafuta mashtaka yanayohusiana na hicho kibali cha DPP, hivyo hoja yetu hakuna ridhaa ya DPP kwa sababu kibali hicho si sahihi,” alidai Kibatala

Alidai shtaka la nne, tano, sita na saba kufunguliwa kwake kunahitaji ridhaa ya DPP na kwa kuwa haipo aliomba yafutiliwe mbali.

 Kibatala alidai hati ya mashtaka ina upungufu kwa sababu shtaka la pili na la tatu hayana maelezo ya kutosheleza ya kuwapa msingi na uwezo washtakiwa kujitetea kikamilifu kijinai. Alidai katika shtaka la kufanya mkusanyiko bila kibali aliwataja hata watu waliotishiwa na kwamba wametajwa kwa wingi hivyo haijulikani ni washtakiwa au ni watu wengine

Kibatala alidai mashtaka yanayowakabili wateja wake yamejichanganya, hayaonyeshi walisababishaje kifo cha Akwilina Akwilini, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na majeruhi walijeruhiwa na nani na kwa kutumia nini

“Maelezo ya shtaka yamerundika vitu vingi kiasi kwamba ni vigumu mtu kujitetea na kwamba unapomshtaki mtu kwa kusababisha kifo ni lazima utoe maelezo ya kutosha kuonyesha unamaanisha kitu fulani ili mtu aweze kujitetea,” alidai.

 Alidai hati ya mashtaka ina upungufu kwa kuwa haionyeshi dhumuni la pamoja ambalo washtakiwa walikutana kulitenda hivyo linawanyang’anya haki ya kujitetea.

 Alidai pia kuna upungufu wa kisheria kwa kuwa mashtaka hayaonyeshi watu waliochochewa kufanya makosa ni kina nani waliohudhuria mkutano, wakazi wa Kinondoni au wapigakura bila kujali itikadi zao

Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alipinga hoja hizo za utetezi na kuiomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hizo

Kuhusu kibali cha DPP kinachoipa Mahakama ridhaa ya kusikiliza kesi, Kadushi alidai hakuna uamuzi wowote ulioweka msingi kwamba ni lazima kiwepo au kisiwepo

Akiahirisha kesi hiyo, hakimu Mashauri alisema atatoa uamuzi kuhusu pingamizi hizo Juni 11, mwaka huu

Mbali na Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, washtakiwa wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu mkuu wa chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu; na wa Bara ambaye pia ni mbunge wa Kibamba, John Mnyika

Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko; katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda, Ester Bulaya.

Kesi ya kina Mbowe yanguruma mpaka saa mbili usiku Kisutu Kesi ya kina Mbowe yanguruma mpaka saa mbili usiku Kisutu Reviewed by KUSAGANEWS on May 16, 2018 Rating: 5

No comments: