Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amefungua barabara ya lami ya Iringa –
Migoli – Fufu yenye urefu wa kilometa 189 na ambayo inaunganisha Mkoa wa Iringa
na Mkoa wa Dodoma.
Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri (The Great North Road) imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 207.457 ikiwa ni ufadhili wa benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania imetoa asilimia 12.8.
Barabara hiyo ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya kuanzia Cape Town nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri (The Great North Road) imejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 207.457 ikiwa ni ufadhili wa benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa asilimia 65.9, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa asilimia 21.3 na Serikali ya Tanzania imetoa asilimia 12.8.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kukamilika kwa barabara
hiyo kumeondoa adha iliyowakumba wananchi kwa miaka mingi ambapo safari ya
Iringa – Dodoma iliyochukua siku nzima ama siku kadhaa wakati wa mvua, sasa
inachukua muda wa saa 2:30.
Balozi wa Japan hapa nchini Mhe.
Masaharu Yoshida na Mwakilishi wa AfDB Bw. Jeremy Aguma wameipongeza Serikali
ya Tanzania kwa utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na taasisi zao, na
wameahidi kukuza zaidi ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
itakayosaidia kukuza uchumi wa wananchi kama inavyoelekezwa katika dira ya
maendeleo ya mwaka 2025.
Wabunge wa Mkoa wa Iringa
wakiongozwa na Mbunge wa Ismani na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mhe. William Vangimembe Lukuvi wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
juhudi zake zilizoyawezesha majimbo yao kupata miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi
wa barabara, vituo vya afya na zahanati, Maji, uwanja wa ndege wa Nduli, Umeme,
ruzuku ya elimu na dawa.
Akizungumza na wananchi
waliojitokeza katika ufunguzi wa barabara hiyo Mhe. Rais Magufuli amewapongeza
kwa kupata barabara ya uhakika na amewataka kuongeza juhudi katika uzalishaji
mali hasa katika kilimo na biashara ili waweze kunufaika nayo.
Mhe. Rais Magufuli amezishukuru AfDB
na JICA kwa kuendelea kuwa washirika muhimu wa maendeleo ya Tanzania, na kwa
namna ya pekee amempongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale
kwa uchapakazi wake, ubunifu, uaminifu na uadilifu uliomwezesha kuiongoza
TANROADS kwa mafanikio hasa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa
barabara na madaraja.
Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na
kujenga barabara hiyo, Serikali inauboresha uwanja wa ndege wa Nduli ili uweze
kupokea ndege kubwa zitakazoleta watalii wengi na wafanyabiashara katika mkoa
wa Iringa na maeneo mengine ya kusini mwa Tanzania ili rasilimali zilizopo
katika maeneo hayo ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ziwanufaishe wananchi kama
wanavyonufaika wananchi wa Kaskazini mwa Tanzania.
“Ruaha ni hifadhi kubwa, nataka
hifadhi hii iwe kitovu cha utalii, nataka nyinyi ndugu zangu wa Iringa mnufaike
na utalii katika hifadhi hii kama wanavyonufaika kule kaskazini kupitia
Serengeti, watalii wakija hapa wenye hoteli watapata wateja, wenye maziwa
watauza, wenye matunda watauza, wenye mahindi watauza, mtapata hela” amesema
Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewataka
wananchi wa Iringa kuwapuuza wanaodai Serikali inakopa sana, na kueleza kuwa
fedha hizo hukopwa kwa masharti nafuu, riba ndogo na hulipwa kwa muda mrefu, na
kwamba ndizo zinatumika kujenga miundombinu ya kuchochea uchumi.
Pamoja na Mke wa Rais Mhe. Mama
Janeth Magufuli sherehe hizo pia zimehudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Job Yustino Ndugai, Mawaziri, Wabunge kutoka kamati
ya bajeti na kamati ya miundombinu, Maaskofu na viongozi wa vyama vya siasa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Iringa
29 Aprili, 2018
Rais Magufuli Alivyofungua Barabara ya lami ya Iringa – Migoli – Fufu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 29, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 29, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment