MWALIMU ALIYEFUNDISHA MIAKA 17 AKIWA HAJUI KUSOMA, KUANDIKA


HUENDA ikawashangaza wengi lakini ukweli ndiyo huo. John Corcoran, mzaliwa wa New Mexico, Marekani, licha ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu na kisha kupata kazi ya ualimu aliyoifanya kwa miaka 17, hakuwa akijua kusoma wala kuandika.
Akisimulia mkasa huo, Corcoran (81), ambaye ni mtoto wa sita katika familia yao, anasema kuanzia mwaka 1961 alipoanza kufundisha hadi alipoacha kazi hiyo mwaka 1978, alikuwa makini kuitunza siri yake hiyo, akihofia kufukuzwa kazi na kujidhalilisha.
“Nikiwa darasa la pili, tulitakiwa kujifunza kusoma. Lakini kwangu ilikuwa ni kama kufungua gazeti la Kichina na kulitazama tu. Sikuwa nikielewa chochote na hata nilipokuwa na umri wa miaka sita, saba na hata nane, bado sikuweza hata kutamka maneno,” anasema.
Anasema kila ilipofika usiku, alimuomba Mungu amwezeshe kusoma ifiakapo asubuhi, akiongeza kuwa aliweza hata kuamka, kuwasha taa na kushika kitabu ili kuona kama Mungu amejibu maombi yake.
Corcoran anasema hali hiyo ilimfanya kuwa kimya kila alipokuwa katika kundi la wanafunzi wenzake ambao wengi walishauaga ‘umbumbumbu’.
Akiwa haelewi hili wala lile, siku moja alishangaa kuona mwalimu wa darasa lao akimwita mzazi wake na kumwambia: “Ni kijana mwenye akili, atasonga mbele kwenda darasa jingine.”
Licha ya kuwa bado hakuweza kusoma wala kuandika, jambo ambalo daima lilibaki kuwa siri yake, Corcoran alishangaa mwalimu wake akiendelea kumvusha na mwishowe kufika darasa la tano.
“Hadi nafika hapo, tayari nilishakata tamaa ya kujua kusoma. Niliweza kuamka asubuhi, nikavaa, lakini kwenda shule ilikuwa ni kama kwenda vitani. Nililichukia darasa. Yalikuwa ni mazingira magumu kwangu na nilifikiria hata namna ya kuyaepuka,” anasema.
Anaongeza kuwa hadi kufikia darasa la saba, alishachoka maisha ya shule na alitamani hata kufukuzwa, japo moyo wake ulimsuta. “Sikutaka kuwa hivyo. Nilitaka kuwa mtu mwenye mafanikio, nilitaka kuwa mwanafunzi bora lakini sikuweza,” anasema.
Corcoran anasema hadi kufika elimu ya juu ya sekondari, aliweza kuandika jina lake tu lakini si sentesi nzima kama wenzake. “Nilikuwa elimu ya juu lakini nilikuwa nasoma vitabu vya darasa la pili na la tatu.  Tulipokuwa tukipewa mitihani, nilikuwa nikichungulia kwa wenzangu au niliweza kumpa mtu karatasi ili aniandikie majibu,” anasema.
Kwa maelezo yake, mambo yalizidi kumuwia magumu zaidi alipofaulu na kwenda elimu ya chuo. Anasema huko alilazimika kuwa karibu na wanafunzi wenye tabia ya kukariri mitihani iliyopita, wakiamini waalimu wao wangerudia baadhi ya maswali.
“Siku moja, kulikuwa na mtihani. Profesa aliingia na kuandika maswali manne ubaoni. Nilikuwa dawati la nyuma, karibu na dirisha.
“Nikanakiri maswali yote ambayo hata hivyo sikujua yalikuwa yanachouliza. Nje ya dirisha, nilishampanga rafiki yangu, ambaye licha ya umri wake mdogo alikuwa ‘kichwa’.
“Nilikuwa napitisha kitabu changu dirishani na ananipa majibu. Wakati wote huo, nilikuwa najifanya naandika ili nisigundulike,” anaongeza.
Anafichua siri zaidi kwamba malipo yake kwa rafiki yake huyo hayakuwa fedha bali ni kumsaidia kutongoza msichana aliyeitwa Mary ambaye pia alikuwa akisoma chuoni hapo.
Anaikumbuka siku nyingine aliyowahi kwenda katika ofisi za profesa chuoni hapo kwa lengo la kuiba mtihani, jaribio ambalo hata hivyo liligonga mwamba, kabla ya kuwashirikisha wenzake na kulikamilisha.
“Kulikuwa na zaidi ya nakala 40 za mtihani, nakumbuka ilikuwa ya maswali ya kuchagua. Hapo nikaona lililoshindikana limewezekana.  Nilianza kuuamini uwezo wangu,” anasema.
Kwa kipindi chote hicho, muda mwingi akiwa peke yake aliutumia kulia, akiumizwa na kitendo cha kutokujua kusoma na kuandika.
“Walimu na wazazi wangu walikuwa wakiniambia kuwa watu wenye Shahada  hupata kazi nzuri, huwa na maisha bomba. Hata hivyo, mimi shida yangu ilikuwa kujua kusoma tu, kwa njia yoyote ile,” anasema.
Bahati mbaya kwake ni kwamba alipohitimu elimu yake ya chuo, akiwa bado hajui kusoma wala kuandika, kulikuwa na uhaba wa walimu wa elimu ya juu ya sekondari, hivyo akachaguliwa kuianza haraka kazi hiyo.
“Hapo unaweza kuona hali iliyonikuta. Yaani nimetoka katika banda la simba, halafu sasa natakiwa kwenda kumuwinda.
“Ilinivuruga kwa kweli. Lakini kwa upande mwingine, niliona ualimu ni sehemu nzuri ya kujificha. Niliamini hakuna atakayefikiria kuwa mwalimu anaweza kushindwa kusoma.
“Bahati nzuri, nikachaguliwa kuwa mwalimu wa michezo. Niliweza kuchapa (kuandika kwa kompyuta) lakini sikujua ninachokiandika. Nilikwepa kuandika ubaoni. Nilipendelea ufundishaji wa kutumia video na majadiliano.
“Mara nyingi nilikuwa na wanafunzi wawili au watatu hivi, ambao walikuwa wanajua kusoma na kuandika vizuri, walikuwa wakinisaidia. Hata hivyo, hawakuwa wakijua kama sijui kusoma. Unawezaje kumshuku mwalimu?” anasema.
Anakumbuka kuwa kati ya changamoto kubwa alizokuwa akikutana nazo shuleni hapo ni kuhudhuria vikao vya idara na walimu wenzake ambavyo vilikuwa vikifanyika kila wiki.
Mbaya zaidi kwa upande wake, mawazo yaliyokuwa yakijadiliwa yaliandikwa ubaoni, jambo ambalo lilimpa wakati mgumu. “Kila nilipohudhuria, nilikuwa nikihofia kuwa nitaitwa lakini nilikuwa najipanga kukabiliana na hali hiyo endapo ingetokea,” anaongeza.
Kwa mujibu wa mwalimu huyo, ilikuwa hatari zaidi alipooa, kwani aliona kuwa imani yake ya Kikristo inamtaka kuwa muwazi kwa mkewe, ikiwamo kutomficha chochote.
Siku moja, akiwa na mkewe aliyemtaja kwa jina la Cathy, alijisemea: “Sijui kusoma.” Kauli ambayo hata hivyo mkewe hakuielewa, akidhani amesema hana kiwango kikubwa cha elimu.
“Tulipobahatika kupata mtoto wa kike, tulikuwa na kawaida ya kusoma naye vitabu kila siku. Lakini sikuwa nikitoa sauti, nilizuga kwa kumsimulia hadithi tu ambazo niliziongezea ‘chumvi.’
“Siku moja, wakati tunasoma kitabu cha ‘Rumpelstiltskin’, binti yangu aliniambia: “Husomi kama mama.”
Corcoran anasema hilo lilimshtua mkewe, akikumbuka kuwa mara nyingi alikuwa akimuomba amsaidie kuandika nyaraka za shule.
Licha ya kwamba mwanamama huyo hakulipa kipaumbele suala hilo, Corcoran alijisikia vibaya na kujiapiza kuwa anatakiwa kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.
“Nikiwa na umri wa miaka 47 ikielekea 48, nilimuona marehemu Barbara Bush (mke wa Rais wa Awamu ya 41 wa Marekani, George H. W. Bush), akizungumzia elimu ya watu wazima kupitia televisheni.
“Ilinisadia. Sikuwahi kumsikia mtu mwingine akilizingumzia hivyo nilidhani niko peke yangu mwenye tatizo hilo.”
Anasema ujumbe wa mwanamama huyo ulimpa morali na ndipo alipaochana na kazi ya ualimu mwaka 1978 ili ajikite katika zoezi la kujua kusoma.
Hapa anasimulia alivyoitembelea maktaba moja na kuomba kukutana na mkurugenzi wa program ya kujifunza kusoma.  “Nikapewa mtu, alikuwa na umri wa miaka 65 hivi. Hakuwa mwalimu lakini alipenda kusoma na hakupenda kuona mtu akiwa hajui kusoma.
“Ilinichukua miaka saba kujiona najua kusoma. Nilipoiva, nililia, nililia sana baada ya kujua kusoma. Nilikuwa na maumivu makubwa,” anasema.
Aidha, kutokana na mateso aliyopitia, Corcoran, ambaye sasa ni mwandishi wa vitabu, anasema jamii itaweza kuepuka janga la wanafunzi kufeli endapo walimu wataacha kubebeshwa lawama na badala yake waandaliwe vizuri.


MWALIMU ALIYEFUNDISHA MIAKA 17 AKIWA HAJUI KUSOMA, KUANDIKA MWALIMU ALIYEFUNDISHA MIAKA 17 AKIWA HAJUI KUSOMA, KUANDIKA Reviewed by KUSAGANEWS on April 22, 2018 Rating: 5

No comments: