Mtoto wa miaka mitatu, mkazi wa Longuo,
Kilimanjaro, amefariki dunia juzi baada ya kuparuliwa na paka
Kifo cha mtoto huyo, kinafanya idadi ya watu
waliokufa kutokana na kuumwa na wanyama aina ya mbwa na paka wilayani Moshi
kufikia wanne katika kipindi cha siku 30
Bila kutaja jina, Ofisa Afya wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Jornas Mcharo alisema mtoto huyo alifikishwa hospitali, Aprili 2
akiwa na dalili za kichaa cha mbwa
Akieleza ni kwa nini mtoto huyo alionekana
kuwa na virusi vya rabbies, (kichaa cha mbwa) wakati ameparuliwa na paka,
Mcharo alisema kwa kawaida ugonjwa wa kichaa cha mbwa unatokana na kukwaruzwa
na wanyama wenye damu za moto. Alisema imezoeleka kuitwa kichaa cha mbwa lakini
husababishwa na wanyama wote wenye virusi hivyo
“Wanyama hao ni wale wenye virusi kama mbwa,
paka, panya, mbweha na popo au hata binadamu mwenye maambukizi ya virusi
hivyo,” alisema
Alisema huo ni miongoni mwa magonjwa
yanayoambukiza binadamu na wanyama yanayojulikana kama (zoonotic diseases
Kuhusu mtoto huyo, Mcharo alisema baada ya
matibabu yake kushindikana katika vituo vya afya, alihamishiwa Hospitali ya
Rufaa ya KCMC lakini alipoteza maisha juzi wakati akipatiwa matibabu
Alisema mtoto huyo baada ya kuparuliwa na
paka, hakupata matibabu mapema hadi baada ya wazazi wake kuona hali yake
inakuwa mbaya, ndipo wakampeleka hospitali. Ilibainika kuwa familia ya mtoto
huyo inafuga paka saba
“Kitu cha kushangaza kidogo, katika mtaa huo
wa Longuo A, familia nyingi zinafuga paka zaidi ya watano, sasa hii ni hatari
kwa kuwa hawajachanjwa na watoto wanacheza na paka bila kujua kama kuna hatari
yoyote inayoweza kutokea,” alisema
Ofisa Afya Manispaa ya Moshi, Mgeta
Sebastian alisema kati ya Januari hadi sasa, watu 201 wameng’atwa na mbwa
katika manispaa hiyo, huku mbwa 113 wakipewa chanjo na 204 wakiuawa
Alizitaka familia kuwapa chanjo wanyama
wafugwao majumbani na kuwapeleka hospitali mapema watu wanaojeruhiwa na wanyama
hao.
Mtoto afariki kwa kuparuliwa na paka Kilimanjaro
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 05, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment