Vuguvugu la maandamano yanayoratibiwa kwenye
mitandao ya kijamii kufanyika Aprili 26, limesababisha watu watatu jijini Tanga
kushikiliwa na polisi wakituhumiwa kuyaratibu
Hata hivyo, Polisi imesema hakuna maandamano
yoyote yaliyoruhusiwa kufanyika siku hiyo na kutahadharisha kuwa yeyote
atakayeandamana asije akawalaumu askari au Serikali kwa sababu atakuwa
‘amelamba sumu’
Akizungumza kamanda wa
Polisi Mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema wanaoshikiliwa walikamatwa maeneo
tofauti jijini Tanga baada ya kufuatiliwa na kubainika kuwa wanahamasisha
maandamano kwenye mitandao ya kijamii
“Tayari watu watatu waliohamasisha
maandamano haya kupitia mitandao ya kijamii tunawashikilia na wapo wengine
ambao tunawafuatilia, tutawakamata wakati wowote kwa kuwa tunazo taarifa zao na
mbinu wanazotumia,” alisema Kamanda Bukombe
Aliwataka wakazi wa Tanga kuondoa hofu
kwamba kutakuwapo na maandamano hayo kwa sababu jeshi limejiandaa
kumshughulikia kila atakayethubutu kuandamana
Machi 21, Polisi Mkoa wa Dodoma iliwakamata
na kuwashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuhamasisha maandamano kwenye
mitandao ya kijamii Aprili 26
Zuio la mkutano
Tishio hilo la maandamano limesababisha Polisi katika Wilaya Masasi, Mtwara kuzuia ziara ya mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe katika Kata ya Lukuledi kwa maelezo kuwa jeshi hilo sasa lipo katika hali ya tahadhari (standy by) kujiandaa na sherehe za Muungano, Aprili 26.
Alipoulizwa iwapo hali hiyo ya tahadhari ni kwa nchi nzima, msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa alisema kila kiongozi ndani ya jeshi hilo kuanzia IGP hadi kwa kiongozi ndani ya wilaya (OCD) ana mamlaka yake katika eneo lake
“Suala si la kitaifa au vipi, jua tu kuwa
kila mmoja ana mamlaka katika eneo lake, kama jambo limetangazwa mkoani waulize
viongozi wa polisi katika mkoa husika, kama yeye ameelezea sababu za kufanya
hivyo ndizo hizo, huku unauliza nini tena,” alihoji Mwakalukwa
Katika barua ya OCD, Moshi Sokoro kwa Mwambe
ambayo Mwananchi imeiona ilieleza kuwa mkutano huo umezuiwa kutokana na
shughuli hiyo ya kitaifa kwa sababu hakutakuwa na askari wa kutosha kuratibu
ziara na kusimamia mkutano huo
Aprili 20, Mwambe aliomba kufanya mkutano
akiambatana na viongozi wengine wa Chadema ngazi ya taifa, Kanda ya Kaskazini,
mkoa na wilaya. Siku iliyofuata alijibiwa kuwa ziara hiyo imekataliwa
Nakala ya barua hiyo inaonyesha ilipelekwa
kama taarifa kwa kamanda wa polisi Mkoa wa Mtwara; mkuu wa upelelezi mkoa huo;
mkuu wa Wilaya ya Masasi na mkuu wa Usalama wa Taifa wa Wilaya ya Masasi.
Mpelelezi wa makosa ya jinai wa Wilaya ya Masasi alipewa nakala kwa ajili ya
utekelezaji
Polisi watano wajeruhiwa Tanga
Katika hatua nyingine, askari watano wa
kitengo cha upelelezi Tanga wamejeruhiwa baada ya gari la Polisi aina ya Land
Rover 110 kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania lenye trela wakati
magari hayo yakipishana katika barabara ya Tanga-
Horohoro
Kamanda Bukombe
alisema jana kuwa ajali hiyo ilitokea jana saa saba mchana karibu na daraja la
Mto Utofu wakati askari hao wakielekea kwenye majukumu yao ya kikazi. Askari
hao ni Sajenti Henry, Konstebo Jafary dereva wa gari la Polisi, Konstebo
Barnabas, Konstebo Fatuma na Konstebo Obed.
Alisema dereva wa lori alikimbia na polisi
wanaendelea kumsaka.
Maandamano mtandaoni yawaponza watatu Tanga
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment