Jonas Kamaleki- MAELEZOSerikali ya Israel imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kurejesha uhusiano unaolenga kuziimarisha nchi hizi mbili kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe. Ayelet Shaked wakati wa Kongamano la Tano la Biashara na Uwekezaji kati ya Israel na Tanzania.
“Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa
kufungua ubalozi wa Tanzania nchini kwetu na tunataraji kuuzindua rasmi juma
lijalo”, alisema Waziri Shaked.
Ameongeza kuwa kwa zaidi ya miongo
minne Tanzania na Israel hazikuwa na mahusiano ya kiuchumi wala ya kisiasa na
kuongeza kuwa sasa nchi yao iko tayari kuwekeza nchini.
Waziri huyo ameeleza kuwa ni mara
yake ya kwanza kufika Afrika na yuko tayari kuja na familia yake kwa ajili ya
kufanya utalii Zanzibar na kwenye mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewakaribisha waisraeli kuwekeza nchini
kwani Tanzania ni kitovu cha uwekezaji kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa
Afrika kutokana na amani iliyopo. Pia ameitaja nchi hii kuwa ni lango la
biashara kwa nchi za kiafrika zinazoizunguka.
“Israel mnakaribishwa kuwekeza hapa
Tanzania kwani mazingira ya uwekezaji ni mazuri, tunayo ardhi nzuri kwa kilimo,
tunayo maziwa, mito kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji, hivyo hakuna
mtakachokikosa endapo mnataka kuwekeza kwenye kilimo”, alisema Waziri Mwijage.
Waziri Mwijage amesema Tanzania iko
tayari kwa uwekezaji katika kilimo, viwanda vya dawa, TEHAMA, utalii,
uzalishaji wa sukari na uongezaji thamani kwenye madini, na hivyo
kuwahakikishia kuwa Serikali inaunga mkono suala la uwekezaji.
Naye balozi wa Israeli kwa nchi za
Tanzania , Kenya, Uganda, Malawi na Shelisheli, Mhe. Noah Gal Gendler amesema
Serikali ya Rais Magufuli imeonyesha mabadiliko makubwa ya ushirikiano wa
kisiasa na kiuchumi kwa muda mfupi.
“Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 46
hakuna waziri hata mmoja kutoka Israeli amewahi kuitembelea Tanzania, lakini
ndani ya wiki mbili wamefika mawaziri wawili toka nchini mwetu”, alisema
Gendler.
Ameongeza kuwa katika kuimarisha
sekta ya Afya, Israeli itajenga wodi za wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum
(ICU) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma, na kituo huduma kwa watoto
katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Kongamno hili ni la tano kufanyika
hapa nchini likiwa na lengo la kuonyesha fursa za uwekezaji zitakazotekelezwa
baina ya wafanyabiashara wa Israeli na Tanzania. Kongamano hili ni fursa kwa
sekta binafsi kuitumia vizuri ili kuongeza tija katika biashara hususan katika
kilimo na uwekezaji katika ujenzi wa viwanda.
Israel Yampongeza Rais Magufuli
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment