Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon
Sirro ametoa onyo akisema wamejiweka tayari kukabiliana na watu, wakiwemo
wanasiasa wanaohamasishana kuandamana nchi nzima kinyume cha sheria.
Sirro alisema hayo jana mjini Bariadi baada ya kukutana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Simiyu alikokuwa ziarani kukagua utayari wa askari wa jeshi hilo
“Kuna makundi ya vijana wanaojiita wana
mapinduzi wanahamasishana na kupanga kuandamana nchi nzima wakiratibiwa na
chama kimoja cha siasa, tumejipanga kuwadhibiti na tutawakamata wote bila
kujali vyeo na madaraka yao,” alisema.
Wakati IGP Sirro akitoa onyo hilo, Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwazungumzia
wanaosambaza ujumbe wa kuwahamasisha wananchi kuandamana kwenye mitandao ya
kijamii akisema watachukuliwa hatua za kisheria
Kamanda Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema Jeshi la Polisi haliwezi kukubali kuona watu hao wanaiingiza nchi katika matatizo na kusababisha amani kupotea
“Wananchi msikubali kutumiwa, hawa
wanaohamasisha baadaye wanakaa pembeni na kuwaacha mnaingia kwenye matatizo.
Watakaojaribu kuandamana tutawakamata na kuwachukulia hatua, hatuwezi kukubali
watu wachache kutuvurugia amani ya nchi,” alisema Mambosasa.
Sirro kwa upande wake aliwataka wazazi na
walezi kuwaonya na kuwazuia vijana wao kushiriki maandamano yasiyo na kibali
kwa sababu hakuna atakayevunja sheria atakayesalimika bila kuchukuliwa hatua
stahiki
“Kuvunja sheria ni jambo rahisi lakini
madhara yake ni makubwa. Wananchi wasijiingize kwenye mambo yakiwemo uhalifu
ambayo mwishowe huwagharimu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mambosasa alisema
polisi inawashikilia watu wawili wakituhumiwa kuhusika na kifo cha aliyekuwa
katibu wa Chadema Kata ya Hananasif, Daniel John.
Alisema Februari 23 saa 5:30 usiku eneo la
Hananasif, polisi waliwakamata mwanamke na mwanamume wanaodaiwa kuhusika na
kifo cha John
“Tunapoletewa malalamiko lazima tuyafanyie
kazi hivyo tulianza uchunguzi juu ya mauaji hayo, hatuwezi kutaja majina kwa
kuwa tunaendelea na upelelezi ili kujua mtandao wote,” alisema Kamanda
Mambosasa.
Akizungumzia uchunguzi kuhusu kifo cha
aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina
Akwilini aliyepigwa risasi Februari 16 wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa
Chadema waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya msimamizi wa uchaguzi wa
ubunge Jimbo la Kinondoni, alisema unafanyika kama ilivyo kwa kesi nyingine.
Kamanda Mambosasa alisema kuuawa kwa
mwanafunzi huyo ni matokeo ya maandamano ya wanachama wa Chadema eneo la
Mkwajuni
Alisema polisi pia imemkamata mkazi wa
Kinondoni, Rajabu Mohamed (25) maarufu Rajeshi akituhumiwa kuwakamata wanawake,
kuwaingiza kwa nguvu kwenye gari lake, kuwapora na kuwafanyia vitendo vya
ukatili
Mambosasa alisema mtuhumiwa alikamatwa
Kinondoni akituhumiwa kuwapata wanawake kwa kuwalaghai kuwa yeye ni
mfanyabiashara
Alisema baada ya kuwapora wanawake mtuhumiwa
huyo huzunguka nao akiwatisha kwamba yeye ni freemason na ana uwezo wa kuwaua
kwa kuwanyonya damu au kuwakata viungo vya miili yao
“Kupitia vitisho hivyo wanawake walilazimika
kutoa neno la siri la simu zao, alichukua kadi zao za benki na kuwaibia fedha
kupitia mashine za kutolea fedha (ATM),” alisema Kamanda Mambosasa
IGP SIRO TUMEJIPANGA KUTHIBITI MAANDAMANO
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 27, 2018
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 27, 2018
Rating:


No comments:
Post a Comment