HALINI MBAYA KWA WATOTO WA KIUME KWA KUFANYIWA UKATILI

Wakati nguvu ya ulinzi ikiwekwa kwa mtoto wa kike, imeelezwa hali ni mbaya zaidi kwa wa kiume kutokana na ukatili wanaofanyiwa ikiwemo kulawitiwa.

Wakizungumza katika kampeni ya ‘Tumkumbuke na Mtoto wa Kiume’ inayoongozwa na taasisi ya Dahuu Foundation, baadhi ya walimu wamesema yapo matukio mengi ya watoto wa kiume kufanyiwa ukatili wa kijinsia, huku jamii ikiwapa kisogo kwa kutowasikiliza.

Mwalimu wa Shule ya Msingi Mivinjeni, Manispaa ya Ilala, Kiemena Athumani amesema wazazi wengi wamejisahau kwa kumuhofia zaidi mtoto wa kike wakiamini wa kiume yupo salama.

 “Nina mifano dhahiri ya watoto kufanyiwa ukatili huu, matukio haya yapo na hufanywa na ndugu wa karibu majumbani kama vile wajomba, kaka na hata majirani,” amesema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muhimbili, Jovitha Mushi amesema matukio mengi huwafika watoto wa kiume bila kujua kwa sababu jamii imejikita zaidi kumkumbatia mtoto wa kike.

Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Ilala, Rehema Msologonhe amesema kuna hatari ya kupoteza akina baba bora siku za usoni kama hali iliyopo itakaliwa kimya.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amewataka wahusika wakiwemo wa madawati ya jinsia kutowafumbia macho watuhumiwa wa kesi za ulawiti na ubakaji.

Amesema kuna hatari ya kuwapoteza vijana wenye nguvu kama wazazi hawatakuwa karibu na watoto wa kiume kwa kuwakumbatia wa kike pekee.

Awali, Mkurugenzi wa Dahuu Foundation, Husna Abdul alisema wameanzisha kampeni ya kumkumbuka mtoto wa  kiume baada ya kufanya tafiti shuleni na kugundua hali ni mbaya.

“Watoto wengi wanafanyiwa ukatili na wazazi wao hawajui chochote kwa sababu hofu yao kubwa wameiweka kwa watoto wa kike peke yao, hii ni hatari,” amesema.

Mwanasheria wa kujitegemea, Jebra Kambole amesema kuna haja kwa Serikali kuandaa muswada wa sheria zitakazowalinda watoto wa kiume dhidi ya ukatili kama ilivyo kwa wa kike.

 
HALINI MBAYA KWA WATOTO WA KIUME KWA KUFANYIWA UKATILI HALINI MBAYA KWA WATOTO WA KIUME KWA KUFANYIWA UKATILI Reviewed by KUSAGANEWS on January 25, 2018 Rating: 5

No comments: