Muungano wa Super Alliance (Nasa) unasema una matumaini makubwa kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) 'ikilainisha mambo' kinara wake Raila Odinga ndiye ataibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Jumanne Agosti 8, 2017
MUUNGANO wa National Super Alliance (Nasa) unasema una matumaini makubwa kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) 'ikilainisha mambo' kinara wake Raila Odinga ndiye ataibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo Jumanne Agosti 8, 2017.
Mkurugenzi wa Nasa na ambaye pia ni kinara mwenza katika muungano huo Musalia Mudavadi amesema kuwa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC inafaa kutoa mwelekeo kamili unaoonyesha kwamba Raila ndiye ameibuka mshindi.
"Tumepata habari kutoka kwa wanaotujuza kwenye IEBC na Raila amepata kura 8,041,726 huku Uhuru Kenyatta akipata kura 7,755,428 lakini matokeo haya yamebadilishwa yakawa Kenyatta amepata kura 8,056,855 naye Raila akipata kura 6,659,493," amedai Mudavadi akihutubu Alhamisi jioni mtaani Westlands jijini Nairobi.
Hata hivyo kinara huyu ambaye pia ni kiongozi wa ANC, amekataa kufichua wanaofahamisha Nasa akihoji kuwa wanataka kubana majina yao.
"Kufuatia swala la Chris Msando, hatutafichua majina ya wajuzi wetu," amesema.
Msando alikuwa kaimu meneja wa mawasiliano katika IEBC japo aliuawa katika hali ya kutatanisha.
"Korti ikiagiza tuwafichue, mawakili wetu watakabiliana na swala hili," ameeleza Musalia.
Matokeo ya kura yanayoendelea kuhesabiwa na kupeperushwa na IEBC kutoka kwenye kituo kikuu cha kujumuisha kura na kutangaza mshindi katika ukumbi wa Bomas of Kenya jijini Nairobi, yanaonyesha Rais Kenyatta wa Jubilee anaongoza kwa kura 8,114,291 naye kinara wa Nasa Raila akizoa kura 6,716,552.
Muungano wa Nasa aidha unataka IEBC isitishe kupeperusha matokeo hayo.
"Tunataka watangaze Mheshimiwa Raila Amollo Odinga kuwa Rais na Bw Kalonzo Musyoka Naibu wake," Musalia ameeleza.
"Raila atazungumza baada ya IEBC kutangaza rasmi matokeo," akafichua.
Ghasia
Nasa aidha imekanusha kuwa kupitia madai yake itachochea ghasia kwa Wakenya.
"Hatuzui ghasia, wala hatufanyi kazi ya IEBC lakini matokeo wanayopeperusha si halali," ameteta.
"Utendakazi wa IEBC unasalia kwao, tutapeana mwelekeo wetu baada ya matangazo kutolewa," akaongeza.
Nasa imeshikilia kuwa mashine za IEBC zilidukuliwa ili kumsaidia Rais Kenyatta kuibuka mshindi jambo ambalo mwenyekiti wa tume hiyo Bw Wafula Chebukati na mkurugenzi mkuu Ezra Chiloba wamepinga vikali, wakisema mashine zao ni salama.
Licha ya Nasa kupatana na wachunguzi wa kimataifa, wamesema kuwa wachunguzi hao hawafahamu kilichojiri. "Ni rahisi kwao kusema uchaguzi ulikuwa wa huru, haki na wazi, lakini hawajui kilichotokea," ameeleza Musalia, akiandamana na kinara wa Nasa Raila, mkewe Bi Ida Odinga, mgombea mwenza Kalonzo Musyoka, Seneta wa Siaya James Orengo na viongozi wengine.
Wachunguzi wa kitaifa kama vile; Common Wealth, muungano wa Afrika (AU), EAC na wengine mapema Alhamisi walidokeza kuwa uchaguzi ulikuwa wa huru, haki na wazi.
No comments:
Post a Comment