Jeshi la polisi Mkoani Mwanza linamshikilia kijana Fabian Jackson, mkazi wa Mahina (32) kwa kumkuta na noti 20 za bandia zenye thamani ya shilingi laki mbili kitendo ambacho ni kosa la jinai.
Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi inasema kwamba polisi wakiwa kwenye doria na misako walipokea taarifa kwamba katika kijiji cha Kanyara yupo mtu ambaye ameingia kijijini hapo na ana noti bandia nyingi, baada ya askari kupokea taarifa hizo walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi kijijini hapo na kufanya upelelezi na msako wa kumtafuta mtu huyo.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (DCP) Ahmed Msangi ambaye amethibitisha kutokea kwa tukio hilo afafanua kwamba kwa sasa mtuhumiwa wa tukio hilo yupo kwenye uchunguzi na pindi uchunguzi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani na kuongeza kwamba msako wa kuwatafuta watu wengine wanaoshirikiana na mtuhumiwa huyo unaendelea ili kuwatia wote mbaroni.
Hata hivyo Kamanda Msangi amewaonya wananchi wa Mwanza kuacha kutengeneza noti za bandia kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na endapo mtu akikamatwa hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
No comments:
Post a Comment