Mahakama ya Rufaa imefuta ombi la kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga uamuzi waa Mahakama Kuu kufuta shtaka la ugaidi lililokuwa linamkabili Mbunge wa Bukoba mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuhusiana na shtaka la ugaidi.
Baada ya maamuzi hayo ya Mahakama, Mbunge Lwakatare amefunguka na kusema serikali imeona haina nia ya kuendelea na mapingamizi hayo katika Mahakama ya Rufaa na kudai kwake yeye ni jambo ambalo anamshukuru Mungu.
"Kama ilivyokuwa tangu awali na kama ambavyo Mahakama Kuu imeona hakukuwepo na njama zozote hii ni mipango ambayo ilikuwa imefanywa hata sielewi kwa sababu zipi jambo ambalo wataalamu, watafiti watakuja kutueleza siku za mbele kwamba sababu zote zilikuwa ni nini, namshukuru Mungu lakini pia nawashukuru Mawakili ambao wamejitoa kuanzia mwanzo kwani wamefanya kazi kubwa sana" alisema Lwakatare
Aidhaa Lwakatare amesema alikuwa hatarajii maamuzi ambayo yamefanywa na mahakama ya rufaa dhidi yake na kusema ndiyo maana amekuwepo jijini Dar es Salaam kwa takribani wiki nzima kujiandaa kwa kesi hiyo.
"Kwa wafuatiliaji wa kesi hii kama mnakumbuka mtiti uliokuwepo ambapo nilikaa ndani katika mahabusu ya Keko kisha nikaamishiwa Segerea kwa muda zaidi ya miezi minne na nafikiri unakumbuka jinsi kesi hii ilivyokuwa na taswira kitaifa kwanza msafara uliokuwa unanisindikiza mahakamani zaidi ya polisi 50, magari zaidi ya 10 hata nikiwa naenda hospitali wakati naumwa nasikindikizwa hivyo hivyo, hospitali kama Muhimbili wanazuiliwa kufanya shughuli zozote mpaka mimi nitibiwe niondoke ndiyo waanze kuhudumia watu wengine, kimsingi kesi ilikuwa inatisha sana" alisisitiza Lwakatare
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, mwezi Machi 2013 ilimfutia kesi ya makosa ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph, baaadaye Jamhuri ilikata rufaa kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu.
No comments:
Post a Comment