Zanzibar yatemwa CAF

Zanzibar imepokonywa uanachama kamili katika Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kwa madai kuwa utaratibu wa kuipa uanachama huo haukufuatwa.

Visiwa hivyo ambavyo ni sehemu ya Tanzania, vilipewa uanachama kamili mwezi Machi mwaka huu katika mkutano ambao uliambatana na uchanguzi mkuu wa shirikisho hilo, na kufanya wanachama wa CAF kuwa 55.

Rais wa shirikisho hilo, Ahmad Ahmad amesema kuwa Zanzibar haikupaswa kupewa uanachama huo kwa kuwa ni sehemu ya Tanzania, hivyo taifa linalopaswa kutambuliwa kwa mujibu wa vigezo vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika ni Tanzania na siyo Zanzibar

“Walipewa uanachama bila kuangalia hadhi yao kama nchi, ambayo iko wazi, CAF haiwezi kutambua vyama viwili tofauti vya soka kutoka kwenye nchi moja, tafsiri ya nchi inatokana na Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa" Amesema Rais huyo wa CAF, katika mkutano unaoendelea nchini Morocco.

Zanzibar ambayo inajitegemea kisoka chini ya chama chake (ZFA) imedumu na uanachama huo ilioupata chini ya Rais aliyepita, Issa Hayatou kwa miezi minne pekee baada ya ushawishi wa muda mrefu.

Zanzibar yatemwa CAF Zanzibar yatemwa CAF Reviewed by KUSAGANEWS on July 22, 2017 Rating: 5

No comments: