Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema safari ya Watanzania kuachana na nguo za mitumba imewadia kutokana na uwepo wa viwanda vya kutengeneza bidhaa hizo nchini.
Amesema uwepo wa viwanda hivyo pia utasaidia wakulima wa pamba kupata soko la uhakika.
Majaliwa amewataka wakulima walime pamba ya kutosha ili viwanda vipate malighafi.
Waziri Mkuu Majaliwa, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo, Julai 16 amesema hayo alipotembelea kiwanda cha nyuzi cha Namera kilichoko Gongo la Mboto na kiwanda cha nguo cha Nida kilichopo Ubungo, Dar es Salaam jana, Julai 15.
Amesema viwanda vya kutengeneza nguo nchini ni ushahidi tosha kwamba nchi iko njiani kuondokana na matumizi ya nguo za mitumba kwa kuwa nyingi zitakuwa zinatengenezwa ndani na kupatikana kwa bei nafuu.
Majaliwa amesema kwa sasa wanunuzi wa pamba hawana sababu ya kwenda kuuza nje ya nchi, badala yake wauze katika viwanda vya ndani ili vizalishe nguo za kutosha.
“Pamba yote inaweza kuchakatwa nchini, hivyo hakuna haja ya kuiuza nje ya nchi. Natoa wito kwa wakulima walime mazao ya kutosha kwa sababu soko la uhakika lipo na hii ndiyo safari ya mwisho ya mitumba,” amesema.
Waziri Mkuu pia ametembelea kiwanda cha Lake kinachozalisha saruji ya nyati ambako amewapongeza wawekezaji wote nchini kwa kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli za kuifanya Tanzania kuwa ya uchumi wa viwanda.
Katika kiwanda hicho kinachozalisha tani 700,000 za saruji kwa mwaka, ameelezwa kimeajiri watu 2,000 na kinalipa kodi ya Sh81.31 bilioni kwa mwaka.
Waziri Mkuu amewataka watumishi kuwa waaminifu, wafanye kazi kwa weledi na wawe waadilifu.
Majaliwa ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi waishio maeneo ya karibu na vilipo na kulipa kodi kwa wakati na viwango sahihi.
No comments:
Post a Comment