Mwanamke Afariki akiombewa kwa ‘Nabii’ Jijini Arusha.....Dada Yake Amkuta Bila Nguo huku akiwa amenyolewa Nywele na Nyusi
Mwanamke mkazi wa Unga-Limited
jijini Arusha , Lightness Kivuyo ameripotiwa kufa wakati akifanyiwa maombi
nyumbani kwa mchungaji aliyejulikana kama ‘Nabii Rajabu’ eneo la Kwa-Mrombo pia
jijini hapa.
Kwa mujibu wa dada wa marehemu,
Juliana Kivuyo, Lightness alikuwa amesindikizwa nyumbani kwa nabii huyo nyakati
za usiku na mumewe aliyemtambulisha kama Shafii Mohammed na kwamba wakati
akifanyiwa ibada ya maombi, alianguka na kufariki miguuni mwa ‘Mtume,’ huyo.
“Baadaye shemeji alikuja nyumbani
akihema, huku anadai kuwa dada alikuwa kwenye hali mbaya kule kwenye maombi,” alisema Juliana na kuongeza kuwa alitoka mbio kwenda
Kwa-Mrombo nyumbani kwa Nabii Rajab na kumkuta dada yake amelazwa kwenye kochi,
akiwa bila nguo isipokuwa tu khanga alizofunikwa nazo.
Nabii huyo pia anadaiwa kumnyoa
nywele zote pamoja na nyusi za macho wakati akimfanyia ‘huduma,’ hiyo.
Polisi jijini hapa wamethibitisha
tukio hilo wakiongeza kuwa tayari watu wawili wamekamatwa kutokana na kifo
hicho cha ‘maombi tatanishi.’
Aidha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa,
Charles Mkumbo ameongeza kuwa atatoa taarifa kamili mara baada ya kikao chake
na Mkuu wa Mkoa.
Mganga Mkuu katika Hospitali ya Mkoa
wa Arusha ya Mount Meru, Jacqueline Uriwo amekiri kupokea mwili wa marehemu,
lakini akasema, “Kwanza walijaribu kutudanganya kuwa huyo mama alikuwa hai
na kwamba aliletwa kwa ajili ya matibabu, lakini tukagundua kuwa walichokileta
ni mwili mfu, hivyo tukampeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti!.”
Mkurugenzi wa Huduma ya Mazishi
katika hospitali hiyo ya mkoa, Dk Francis Coster alisema mwili ulipelekwa hapo
na mume wa marehemu ambaye alisisitiza kuwa mkewe hajafa, bali kazimia tu na
kwamba mara nyingi huzimia kwa saa nyingi.
Dk Coster aliongeza kuwa ilibidi na
wao wasiweke mwili kwenye jokofu na kuulaza kwenye machela kwa saa sita na
ndipo wakaamua kuuweka kwenye droo za maiti, kwani ilikuwa wazi sasa kwamba
asingeamka tena asilani.
Waganga hospitalini hapo wamekiri
kuwa mwili wa marehemu uliletwa hospitalini hapo ukiwa umenyolewa upara, lakini
ukiwa na mikwaruzo pamoja na uvimbe hususan maeneo ya mikono na kifua.
Baba mkubwa wa marehemu, Ally Kivuyo
ambaye ndiye mlezi wa Lightness, alisema mume wa marehemu alimtaarifu juu ya
kifo hicho na kuongeza; “Lakini baadaye nikaletewa taarifa nyingine kuwa
Lightness kumbe alikufa wakati akifanyiwa maombi au vitu vingine, nyumbani kwa
mtu anayeitwa ‘Nabii Rajabu,’ hapo basi ikabidi niwataarifu polisi ambao
walikuja kumkamata mumewe pamoja na huyo anayejiita nabii au mtabiri.”
Mwanamke Afariki akiombewa kwa ‘Nabii’ Jijini Arusha.....Dada Yake Amkuta Bila Nguo huku akiwa amenyolewa Nywele na Nyusi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
November 18, 2016
Rating:
No comments:
Post a Comment