Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli
amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 483 kwa mwaka huu kwa ajili ya
mikopo ya elimu ya juu ambapo wanafunzi zaidi ya 118,000 watanufaika.
Akizungumza katika uwekaji wa jiwe
la msingi la hostel za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam leo, Rais Magufuli amesema
miongoni mwa hao watakaonufaika, wanafunzi 93,000 ni wanaoendelea na masomo na
wanafunzi takribani 25,000 ni watakaoanza masomo mwaka huu huku akiweka bayana
kuwa mikopo hiyo itatolewa kwa wanafunzi ambao wanatoka kwenye familia
masikini.
Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia kurekebisha dosari zilizopo katika mfumo wa utoaji
wa mikopo ikiwa ni pamoja na upangaji mbaya wa wanafunzi katika vyuo, kutoa
mikopo kwa upendeleo, kutozingatia sifa za mkopaji, kutoa mikopo hewa na
kufungua vyuo kabla ya mikopo ya wanafunzi kutolewa na pia amewaonya wanafunzi
kujiepusha na vitendo visivyofaa wakati Serikali inarekebisha dosari hizo.
"Na ndio maana wakati mwingine
na wabaya wanapitia humo humo, mara fanye hivi fanyeni vile, wakati wanajua
kuwa mkifanya yasiyofaa Serikali itawafukuza tu ili mkafanyie mambo yenu huko.
"Kwa sababu huwezi kuwa
unahangaika kutafuta fedha za kuwapa mikopo, wakati huo huo unahitaji kujenga
reli, wakati huo huo unahitaji kujenga barabara, wakati huo huo unahitaji
kulipa mishahara, wakati huo huo unahitaji kutoa elimu bure, wakati huo huo
Karagwe kuna njaa, wakati huo huo watu wanahitaji dawa hospitali, halafu watu
wengine wanataka kukuendesha kana kwamba hela unayokusanya ni kwa ajili yao tu,
ni lazima tuelewane na mimi ninataka kuwaeleza kwa dhati lazima twende katika
njia iliyonyooka, ni bora uwe Rais usiye maarufu lakini utimize uliyoyaahidi,
asitokee mtu wa kukuendesha, ninajua mmenielewa" amesisitiza Dkt. Magufuli.
Dkt. Magufuli ameiagiza Bodi ya
Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kujipanga vizuri kukusanya marejesho ya mikopo
kwa wote waliokopeshwa na bodi hiyo ambapo mpaka sasa bodi inadai takribani
Shilingi Trilioni 2.6.
Alichosema Rais Magufuli kuhusu mikopo ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 21, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
October 21, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment