SERIKALI
imetangaza msimamo wake wa kutoajiri madaktari watakaotaka kufanya kazi
katika maeneo ya mijini pekee hususan Dar es Salaam, badala yake
imesema itawachukua watakaokuwa tayari kuhudumia wagonjwa katika maeneo
yote ya nchi.
Aidha,
imeonya tabia ya baadhi ya madaktari bingwa kung’ang’ania kufanya kazi
mijini na kusema wanawanyima haki wahitaji wa huduma zao katika maeneo
ya mengine tofauti na mijini.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu alitoa msimamo huo jana bungeni mjini Dodoma, wakati akijibu
swali la nyongeza la Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM)
aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupeleka madaktari bingwa katika
Hospitali ya Mkoa wa Tabora aliyotajwa ina uhaba mkubwa wa madaktari
hao.
Ummy alisema, “Madaktari
wanaoomba kazi wajiandae kutawanywa na wajue kuwa sasa hatutachukua
watakaotaka kukaa mijini hasa Dar es Salaam, kwa kuwa wananchi katika
maeneo mengine yasiyo ya mijini wanahitaji huduma zao pia, hasa
madaktari bingwa wa wanawake.”
Alisema
anatambua changamoto ya uhaba wa madaktari katika hospitali ya mkoa wa
Tabora na kwamba utapewa kipaumbele mwaka huu Serikali itakapoanza
kutekeleza mpango wa kupeleka madaktari bingwa kwenye mikoa tisa nchini.
“Tabora
imefanyiwa tathmini ikabainika ina uhaba wa madaktari, mwaka huu
itapatiwa madaktari kwa sababu tuna mpango wa kuwapeleka katika mikoa
nane na huo sasa utakuwa ni wa tisa na utapewa kipaumbele,” alisema Ummy.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Suleiman Jaffo
wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema),
Raphael Michael alisema, ili kuhakikisha ukarabati wa miundombinu ya
hospitali ya Mawenzi unafanyika, Serikali imetenga Sh bilioni 1.35
katika bajeti yake ya mwaka 2016/17.
Katika
swali lake la msingi lenye vipengele a, b na c, Michael aliuliza ni
lini hospitali hiyo itafanyiwa ukarabati iweze kufanya kazi zake kwa
ufanisi na kuiongezea madaktari na wauguzi.
Aliuza
pia ni lini Serikali itakubali ombi la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi
la kujenga hospitali ya wilaya na je, Serikali itasaidiaje hospitali ya
Mawenzi iweze kupata mkopo kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB),
ili iweze kuboresha miundombinu yake.
Akijibu
alisema, mkoa umejiwekea utaratibu wa kufanya ukarabati wa hospitali ya
mkoa kupitia fedha za uchangiaji gharama za matibabu.
Hadi
sasa zimetumika Sh 14,700,000 kwa ajili ya ukarabati wa mfumo wa maji,
jengo la wagonjwa wa nje pamoja na jengo la madaktari waliopo mafunzoni
na kuongeza kuwa mkakati uliowekwa ni kuimarisha makusanyo ya mapato ili
kujenga uwezo wa kuihudumia hospitali hiyo.
Kuhusu
suala la watumishi, alisema hospitali hiyo imepata kibali cha kuajiri
watumishi wapya 79 katika mwaka 2015/17 na watumishi 65 wamepangwa
kuajiriwa katika mwaka ujao wa fedha ili kukabiliana na upungufu uliopo.
Serikali Kutoajiri Madaktari Watakaotaka Kufanya Kazi Mjini Pekee
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 03, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 03, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment