Magufuli apaisha uwekezaji nchini

KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesema Rais John Magufuli amepaisha kasi ya uwekezaji nchini, ikielezwa ndani ya miezi sita ya utawala wake amevutia wawekezaji wapya 551.

Idadi hiyo ya wawekezaji katika miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 9,211.88 (karibu Sh trilioni 2), ni sawa na ongezeko la asilimia 20.

Miradi hiyo imeandikishwa kuanzia Desemba mwaka jana hadi Mei mwaka huu, ambapo kati ya miradi hiyo 229 sawa na asilimia 42 inamilikiwa na Watanzania na miradi 251 sawa na asilimia 39 inamilikiwa na wageni na miradi 107 inamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni.

Taarifa hiyo imekuja baada ya Jarida maarufu la kila mwezi la Uingereza la Economist, linalochambua masuala ya kiuchumi na kisiasa, katika toleo lake la Mei 2016, kudai katika taarifa yake kuwa tangu Rais Magufuli aingie madarakani, amezorotesha uchumi na ameifanya nchi ionekane kuwa haiwekezeki.

Habari hiyo pia iliandikwa na gazeti la hapa nchini la MwanaHalisi toleo la Mei 30 –Juni 5, mwaka huu.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Meneja Uhusiano wa TIC, Daud Riganda alisema miradi hiyo inaonesha ongezeko la asilimia 20.31 ya miradi, ukilinganisha na kipindi cha miezi sita ambacho Rais Magufuli hakuwepo madarakani.

‘’Kuanzia Juni hadi Novemba mwaka jana, miradi ya uwekezaji ipatayo 458 yenye thamani ya dola za Marekani 5,727.29. Kati ya miradi hiyo, miradi 201 sawa na asilimia 44 inamilikiwa na watanzania, miradi 159 sawa na asilimia 35 inamilikiwa na wageni na miradi 98 (asilimia 21) inamilikiwa kwa njia ya ubia,’’ alisema Riganda.
Magufuli apaisha uwekezaji nchini Magufuli apaisha uwekezaji nchini Reviewed by KUSAGANEWS on June 03, 2016 Rating: 5

No comments: