Professor Johannes Mbusiro Monyo Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha
(IAA) amehukumiwa kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kupatikana
na hatia kwa makosa ya rushwa. Hii ilikuwa baada ya kusikilizwa kwa kesi
iliyokuwa inamkabili toka mwaka 2014.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mhe.
Devota Msofe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Mahakama iliridhika
na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri hivyo tarehe 29/04/2016
mshitakiwa alikutwa na hatia kwa makosa yote aliyoshitakiwa nayo.
Aidha, katika kipindi hicho akiwa anatumikia adhabu hiyo hatakiwi
kufanya kosa lolote la jinai.
Mnamo
tarehe 08.02.2013 Ofisi ya TAKUKURU (M) Arusha ilipokea tuhuma
kuhusiana na Professor Johannes Mbusiro Monyo Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu
Arusha (IAA). Professor Johannes Mbusiro Monyo alikuwa anatuhumiwa kwa
kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume na sheria namba 11/2007.
Taarifa hiyo ilibainisha kwamba mtajwa alijihusisha na vitendo vya
rushwa na kufanikisha kuwapatia ajira za kudumu watumishi wanane (8)
katika chuo hicho wakati akijua kwamba watumishi hao hawakuwa na sifa.
Katika kuthibitisha tuhuma dhidi ya mtuhumiwa, Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana Rushwa ilianzisha uchunguzi na baada ya kukamilisha uchunguzi
huo iliwasilisha jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kisha kilitolewa
kibali cha mtuhumiwa kufikishwa mahakamani kwa kosa la Matumizi Mabaya
ya Madaraka.
TAKUKURU
(M) wa Arusha baada ya kukamilisha uchunguzi tarehe 31/07/2014
ilimfikisha mtuhumiwa mahakamani na kufunguliwa shauri la jinai namba
15630 akikabiliwa na makosa 16 ya matumizi mabaya ya madaraka kinyume na
kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya
mwaka 2007.
Makosa nane ya kwanza kati ya makosa 16 yalikuwa ni ya
kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutumia madaraka yake vibaya hivyo
kuwaingiza katika utumishi wa umma watumishi nane bila ya kupata kibali
kutoka kwa Katibu Mkuu – Utumishi. Watumishi hao ni wafuatao: Pamela
Dismass Maboko, Samsoni Laurance Mbarya, Mawazo Elias Ndaro, Juma Babu
Nyarutu, Lilian Anselim Ngowi, Godfrey Daudi Mollel, Musa Ramadhani
Maiki na Salim A. Shaban.
Aidha,
makosa nane ya pili kati ya makosa 16, yalikuwa ni mtuhumiwa
kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kutumia madaraka yake vibaya kwa
kuwaingiza katika utumishi wa umma watumishi hao hao nane ilihali akijua
fika kwamba wahusika hawakuwa na elimu ya kidato cha nne kiwango
ambacho ni cha chini kabisa kinachohitajika kwa Mtumishi wa Umma
kuajiriwa. Kwa kufanya hivyo mshitakiwa alikwenda kinyume na Sheria ya
Utumishi wa Umma Namba 02 ya mwaka 2002 kama ilivyofanyiwa marekebisho
mara kwa mara.
TAKUKURU
Mkoa wa Arusha inawashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaouonesha kwa
kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa. Aidha, inawatahadharisha
watumishi wote wa Umma na binafsi kuzingatia maadili wakati wa
utekelezaji wa majukumu yao kwani TAKUKURU haitasita kuchukua hatua
stahiki dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa.
IMETOLEWA NA
JUVENTUS M. BAITU
MKUU WA TAKUKURU (M) ARUSHA
5/5/ 2016
MKUU WA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA AHUKUMIWA KIFUNGO
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 06, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 06, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment