WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya dola viimarishe ulinzi
kwenye mipaka ya nchi na hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi ili
kuzuia uingizwaji holela wa mchele wa magendo kutoka nje ya nchi.
Ametoa
agizo hilo leo mchana (Jumatano, Aprili 27, 2016) wakati akijibu hoja
za wabunge na kuhitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na
taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2016/2017 bungeni mjini Dodoma.
“Napenda
kuviagiza vyombo vya dola viendelee kuimarisha ulinzi wa mipaka yetu
hasa katika mwambao wa Bahari ya Hindi ili kuzuia uingizwaji holela wa
mchele wa magendo kutoka nje ya nchi. Endapo patatokea upungufu wa
mchele nchini, Serikali itaangalia uwezekano wa kuruhusu kuagiza mchele
kutoka nje,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema katika kipindi cha miaka sita iliyopita, kumekuwa na
ongezeko la asilimia 14 katika uzalishaji wa mpunga hapa nchini na hivyo
kufanya kiwango cha uzalishaji kiwe ni kikubwa kuliko mahitaji.
“Takwimu
za uzalishaji mpunga zinaonesha kuwepo ongezeko katika kipindi cha
miaka sita iliyopita ambacho kiliongezeka kutoka tani 1,699,825 mwaka
2009/2010 hadi kufikia tani 1,936,909 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko
la asilimia 14. Katika kipindi chote hicho, kiwango cha uzalishaji wa
mpunga kimekuwa kikubwa kuliko mahitaji,” amesema.
“Kutokana
na mwenendo huo mzuri wa uzalishaji wa mpunga hapa nchini, Serikali
ilisitisha kutoa vibali vya kuagiza mchele kutoka nje ya nchi tangu
Machi, 2013. Hatua hii itasaidia wakulima wetu kupata soko la uhakika na
bei nzuri, jambo ambalo linawaongezea kipato na pia kuwahamasisha
kuongeza uzalishaji zaidi,” amesema.
Akizungumzia
kuhusu deni la sh. bilioni 134 ambalo Serikali inadaiwa na Bohari ya
Dawa nchini (MSD), Waziri Mkuu alisema Serikali imeanza kulishughulikia
deni hilo kwa kumwelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) ahakiki deni hilo. “Mpaka sasa CAG amehakiki madai ya jumla ya shilingi bilioni 67 na kazi ya uhakiki inaendelea.”
Akifafanua
kuhusu vigezo vilivyutumika kugawanya majimbo mapya ya uchaguzi, Waziri
Mkuu alisema mwaka 2015, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipokea maombi 77
ya kuanzishwa majimbo mapya, ambapo Halmashauri 37 ziliwasilisha maombi
ya kugawa majimbo ya uchaguzi na maombi 40 yalitoka katika majimbo
yaliyokuwepo yakiomba kugawanywa. Kati ya maombi yaliyowasilishwa,
maombi 35 tu ndiyo yalikidhi vigezo na yalistahili kugawanywa.
“Kutokana
na ongezeko la Halmashauri mpya ambazo kisheria ni majimbo ya uchaguzi,
ongezeko la idadi ya wabunge wanawake wa viti maalum na uwezo wa ukumbi
wa Bunge; Tume iliamua kutumia vigezo vitatu tu ili kupata idadi ya
majimbo yanayoweza kugawanywa. Vigezo hivyo ni: Wastani wa idadi ya watu
(Population Quota), mipaka ya kiutawala na uwezo wa ukumbi wa Bunge,” alisema.
Waziri
Mkuu alisema chini ya mchakato huo, Tume ilianzisha majimbo mapya 25
ambapo majimbo 19 yalitokana na ongezeko la Halmashauri mpya; na majimbo
sita yalitokana na kigezo cha wastani wa idadi ya watu.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu alibainisha kwamba kwa sasa Serikali haina mpango wa
kuongeza maeneo mapya ya utawala zikiwemo wilaya na mikoa mipya kwa
sababu bado inaendelea kujengea uwezo wa rasilmali watu na vitendea kazi
katika maeneo mapya ya utawala yaliyopo hivi sasa.
Bunge limepitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2016/2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980, DODOMA.
JUMATANO, APRILI 27, 2016.
Serikali Yazuia Uingizaji Holela Wa Mchele.
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 27, 2016
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 27, 2016
Rating:


No comments:
Post a Comment