KESI ya
mauaji ya Aaron Nongo mwenye ulemavu wa ngozi (albino) imeanza kusikilizwa tena
leo hii kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza baada ya kusimama kwa miezi
takriban mitano.
Shauri hilo
namba 213 la mwaka 2014 liko mbele ya Jaji Robert Makaramba, ambaye ndiyo
kwanza ameanza kulisikiliza baada ya jaji wa awali, Ashery Sumari, kupewa
uhamisho.
Washtakiwa
katika kesi hiyo walikuwa watano, lakini leo hii mahakama imearifiwa kwamba mmoja
– Paulo Budeba Genji maarufu kama Lumalija – alifariki dunia Novemba 22, 2014 katika
Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, wakati akiwa mahabusu.
Taarifa hiyo
ilitolewa na kiongozi wa mawakili wa upande wa mashtaka, Emil Kiria, ambaye
aliiomba mahakama, akirejea Kifungu cha 284 (a) cha Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai, kwamba inapotokea hali kama hiyo mashtaka dhidi ya mtu huyo
yanafikia kikomo, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama.
Washtakiwa
waliobakia kwenye kesi hiyo ni Chacha Jeremia, Mathew Jeremia Mlimi, Paschal
Lugoye Mashiku na Alex Joseph maarufu kama Bugwema Silola Jangalu.
Kesi hiyo
ambayo inaendelea tena kesho katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, iko katika
hatua ya ushahidi ambapo shahidi wa sita wa upande wa mashtaka atatoa ushahidi
wake.
Leo hii
mashahidi wawili wametoa ushahidi wao na kufanya idadi ya mashahidi
waliokwishatoa ushahidi wao kufikia watano mpaka sasa.
Marehemu Nongo
aliuawa Juni 26, 2009 majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani kwake Ibanda
Relini, jijini Mwanza ambapo wauaji hao walimkata usoni na kisha kumkata miguu
yake yote miwili na kutoweka nayo pamoja na meno mawili ya mbele.
KESI YA MAUAJI YA ALBINO AARON NONGO YAANZA KUSIKILIZWA TENA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 13, 2015
Rating:
No comments:
Post a Comment