Wakati mjadala wa kifo cha ofisa wa polisi anayedaiwa kujinyonga akiwa mahabusu ukipamba moto, mawakili na maofisa wa zamani wa Jeshi la Polisi wametofautiana juu ya uwezekano wa mtu kujinyonga mahabusu.
Tukio hilo, licha ya
kukumbushia matukio mengine ya mahabusu kudaiwa kujinyoga wakiwa mikononi mwa
polisi, limeibua maswali saba yanayolifanya liwe tukio lenye utata na
kitendawili kinachohitaji kuteguliwa.
Licha ya mawakili na
maofisa hao wa zamani kufunguka, madaktari nao wametofautisha kifo kitokanacho
na mtu kujinyonga mwenyewe au kunyongwa na mtu mwingine halafu ionekane
amejinyonga ili kupoteza ushahidi fulani au sababu nyingine.
Grayson Mahembe (26),
mkaguzi msaidizi wa polisi anadaiwa kukutwa amejinyonga katika mahabusu ya
Kituo Kikuu cha Polisi mjini Mtwara asubuhi ya Januari 22, wakati yeye na
maofisa wengine saba walipokuwa wakishikiliwa kwa tuhuma za mauaji.
Maofisa hao
wanatuhumiwa kumuua kwa makusudi mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamisi na kuutupa
mwili wake huko Kijiji cha Hiari wilayani Mtwara ili asifuatilie fedha
walizompora. Mauaji hayo yanasadikika yalifanywa Januari 5, baada ya askari hao
kuchukua Sh70 milioni kutoka kwa mfanyabiashara huyo.
Tayari maofisa saba
waliokuwa wakishikiliwa wamefikishwa mahakamani juzi mchana kwa tuhuma za kuua
kwa kukusudia.
Akizungumzia msiba wa
mwanaye, mama mzazi Hawa Ally alisema bado hawajakabidhiwa mwili kwa ajili ya
mazishi kwani wameambiwa uchunguzi bado unaendelea na watatoa heshima zao za
mwisho pindi jeshi litakapokamilisha utaratibu wa kukusanya ushahidi kwa ajili ya
mashtaka yaliyopo mahakamani.
Wakati taarifa ya
Polisi Mkoa wa Mtwara ikieleza alijinyonga akiwa mahabusu, baadhi ya wananchi
wanahoji ilikuwaje akajinyonga bila watuhumiwa wenzake kuona au kusikia
purukushani.
Tayari ndugu, akiwamo
baba mzazi wa marehemu, Gaitan Mahembe wamelitaka Jeshi la Polisi kuchunguza
kiini cha kifo hicho, wakidai mazingira ya kujinyonga kwake hayawaingii
akilini.
Polisi wastaafu
wafunguka
Ofisa wa Polisi
aliyestaafu akiwa na cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Yusuph Mruma
alisema mtuhumiwa kujiua akiwa mahabusu ni jambo linalowezekana kutegemea
mazingira ya mahabusu aliyomo.
“Hata shati mtu
anaweza kujinyongea. Unataka kuniambia mtu hawezi kujinyonga kwa suruali? Kama
mazingira ya lockup (mahabusu) yanaruhusu kujining’iniza si jambo la kushangaza
kujinyonga,” alisema.
“Lakini hii itatokea
tu kama yuko mwenyewe mahabusu. Kama kuna watuhumiwa wengine watapaza sauti na
CRO atakuja. Haya ya kujinyonga mahabusu mara nyingi ni kama yuko mwenyewe,”
alisema Mruma.
Wakili Hudson
Ndusyepo, aliyewahi kuwa kachero wa polisi, mwendesha mashitaka na sasa wakili
wa kujitegemea, alisema mahabusi kujinyonga akiwa mahabusu ni jambo
linalowezekana kutegemea mazingira.
“Hili linawezekana kwa
sababu ni binadamu, ana mbinu nyingi ikichangiwa na mazingira atakayokuwepo. Ni
angalizo, kabla ya kuingia mahabusu sharti uvue mkanda na usiingie na kitu
kinachoweza kutumika kuleta madhara,” alisema.
Maswali magumu
Wakizungumzia
uwezekano wa mtu kujinyonga akiwa mahabusu, baadhi ya wanasheria, akiwamo
Wakili Peter Madeleka walisema ni jambo lisilowezekana. “Kwa mazingira ya
mahabusu za polisi, kujinyonga ni ngumu sana kwa sababu kabla hujaingia
utatakiwa kuvua viatu, mkanda na utakabidhi mali kama fedha na simu ndipo
utaingia,” alisema Madeleka.
Naye Tito Magoti,
mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) alisema siyo rahisi
kujinyonga ndani ya kituo cha polisi.
“Isitoshe, kama kuna
watu ndani, itawezekanaje wakuone unajinyonga wakuachie?” alihoji Magoti.
Kinachotokea
ukijinyonga
Wakati mjadala
ukiendelea nchini kuhusu mahabusu za polisi kuwa na mazingira yanayomwezesha
mahabusi kujinyonga hadi kufa, madaktari wameeleza kinachotokea mtu
anapojinyonga au kunyongwa.
Dk Kareem Segumba
ambaye ni mkuu wa Chuo cha St John cha Sayansi Shirikishi cha Jijini Mbeya,
anasema kinachosababisha mtu aliyenyongwa au kujinyoga afe ni kuathiriwa kwa
mzunguko wa damu mwilini.
“Tunapoongelea
kujinyonga au strangulation kama tunavyoita kitaalamu ni ile hali ambayo mtu
anajiua kwa makusudi au kundi la watu wanamuua kwa makusudi kutaka kitu fulani
au kupoteza ushahidi,” alisema na kuongeza:
“Mara nyingi watu
wanaojiua wenyewe huwa wanajining’iniza kwenye kitanzi. Sababu inayofanya afe
ni kwamba mishipa mikubwa inayosambaza damu kutoka kwenye moyo inapita kushoto
na kulia mwa shingo. Akijinyonga au kunyongwa, kile kitanzi kinakwenda
kuikandamiza mishipa ya damu kuzuia usambazaji damu kwenda mwilini.”
Kwa maana hiyo,
anasema mapafu yatajaa, damu itakuwa haifiki kwenye ubongo na moyo utasimama
kufanya kazi kwa maana hauwezi tena kufanya kazi. Hili halitokei kwa anayekufa
kwa kitanzi tu, hata akikabwa shingo kwa namna yoyote anaweza kupoteza maisha
iwapo mkabaji atakandamiza hiyo mishipa.
“Hata ukimpiga mtu
kabali kwa muda fulani, atakufa kwa sababu damu itakuwa haifiki kwenye moyo,
ubongo wala mapafu. Ndiyo maana ili kuthibitisha mgonjwa amejinyonga au
amenyongwa, utaona kuna michubuko kwenye shingo halafu ulimi umevimba na mapafu
yamejaa. Tunaangalia hayo tunapofanya postmoterm,” alisisitiza Dk Kareem.
Kwa upande wake, Dk
Issa Mmbaga aliyestaafu Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi na St
Joseph anasema kujinyonga kunahusisha hewa ya oksijeni kutofika kwenye ubongo
na moyo.
Kwa mujibu wa Dk Issa,
hii inatokana na kukandamizwa kwa mshipa unaopeleka damu kichwani, hivyo
kusababisha ubongo kufa.
Jeshi kuchunguza
Jeshi la Polisi
limewataka wananchi wenye ushahidi wa mauaji na unyang’anyi wa fedha za Hamis
kuuwasilisha kusaidia uchunguzi unaofanywa na timu ya makachero wakiongozwa na
Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya Jinai, Camilius Wambura ambaye yuko mkoani
Mtwara kwa siku kadhaa sasa.
“Jeshi la Polisi
linatoa wito kwa mwananchi endapo kuna mwenye ushahidi mwingine wa ziada wenye
kuthibitisha uhalifu mwingine wa wahalifu hao, wawasilishe ushahidi huo kwa
timu hiyo,” ilinukuu sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na msemaji wa Jeshi la
Polisi, David Misime.
Jeshi la Polisi
limesema limeunda timu kuchunguza tukio hilo kwa kukusanya ushahidi
utakaowezesha kuthibitisha tuhuma zinazowakabili askari wake.
“Yanayodaiwa kufanywa
na maofisa na askari hao si maelekezo ya Jeshi la Polisi, bali ni matendo yao
binafsi na tamaa za kutaka kujipatia fedha kinyume cha sheria, kanuni na
taratibu za nchi,” imesema taarifa hiyo ya Misime.
No comments:
Post a Comment