Maofisa saba wa Jeshi la Polisi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Hakimu Mkazi Mtwara, kwa tuhuma ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis aliyekuwa akiishi Nachingwea mkoani Mtwara.
Miongoni mwa
washtakiwa hao ni Gilbert Kalanje, ambaye aliwahi kumtolea bastola Waziri wa
Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye.
Tukio la Nape
kutishiwa kwa bastola lilitokea Machi 23, 2017, baada ya mwanasiasa huyo
kutenguliwa katika wadhifa wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
alipokuwa akijiandaa kufanya mkutano na waandishi wa habari katika Hoteli ya
Protea jijini Dar es Salaam, lakini baadhi ya askari kanzu, akiwamo Kalanje
aliyemtolea bastola walimzuia.
Maofisa wengine
waliotajwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njera ni aliyekuwa Mkuu wa
Kituo cha Polisi Mtwara, Mrakibu Msaidizi wa Polisi Charles Onyango, aliyekuwa
Mkuu wa Intelijensia Mkoa, Mrakibu wa Polisi, Bicolas Kisinza, Mkaguzi wa
Polisi, John Msuya, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Marco Mbota, Mkaguzi wa Polisi,
Shiraz Ally Mkuka na G5158, Koplo Salum Juma Mbalu.
Akizungumza na
Mwananchi jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Lugano Kasebele alisema
washtakiwa walifikishwa mbele yake na kusomewa mashtaka, lakini hawakutakiwa
kujibu chochote.
“Upelelezi bado
haujakamilika, hivyo kesi hiyo itatajwa tena Februari 8, 2022. Upelelezi
utakapokamilika kesi hiyo itapelekwa Mahakama Kuu Kanda ya Kusini kwa ajili ya
kusikilizwa,” alisema Hakimu Kasebele.
Aliongeza kuwa kwa
kuwa shtaka walilosomewa halina dhamana, washtakiwa hao wamepelekwa rumande
katika gereza la Lilungu lililopo wilayani Mtwara.
Mwendesha mashtaka wa
kesi hiyo ni Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wilbroad Ndunguru.
Hata hivyo, miongoni
mwa maofisa wanaotuhumiwa kuhusika na tukio hilo, alikuwa Grayson Mahembe
anayedaiwa kujinyonga hadi kufa akiwa mahabusu, jambo lililozua maswali kuhusu
uwezekano huo huku familia yake ikitaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili
haki iweze kutendeka.
Usalama wa mahabusu
Akizungumzia suala
hilo alipoulizwa na Mwananchi kwa simu jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David
Misime alisema licha ya ofisa huyo kufariki dunia, bado mahabusu za polisi
nchini zina usalama.
“Ni kwamba selo au
mahabusu za polisi zinajengwa katika hali ya kuzingatia masuala ya kiusalama ya
kuhakikisha wanaoingizwa mle wanakuwa salama saa zote. Ndiyo maana wanaingizwa
watuhumiwa maelfu Tanzania nzima na wote wanatoka wakiwa salama.
“Linapotokea tukio
moja huwezi kuhitimisha kwa kusema kuwa mahabusu hizo haziko salama,” alisema
Misime.
Akifafanua zaidi,
Misime alisema; “Tukumbuke anayeingizwa mle wakati mwingine anapo tafakari kosa
alilotenda na kuona ushahidi ulivyo mzito dhidi yake na ni aibu kwake,
anashindwa kuhimili au kuvumilia hali hiyo na ndipo huanza kutafuta mbinu za
kujidhuru, ikiwapo ya kujinyonga au hata kutoroka.
“Pia tukumbuke huyo ni
binadamu, anayo maarifa mengi ya kufanya alilokusudia akipata mazingira mazuri
kama vile mahabusu wenzake wanapokuwa wamelala. Jeshi la polisi linaendelea
kusisitiza kuwa selo au mahabusu katika vituo vya polisi ni salama,” alisema
Misime.
Alipoulizwa kuhusu
uchunguzi wa mwili wa Mahembe kabla hajazikwa mkoani Iringa, Misime alisema kwa
mtu aliyekufa katika mazingira hayo, ni lazima taratibu zote za kisheria
zifuatwe.
“Ikiwepo kuufanyia
mwili uchunguzi wa kitaalamu ambayo kama ulivyosema kuufanyia mwili postmortem
kwa sababu inafahamika fika lazima hilo litaulizwa,” alisema Misime.
No comments:
Post a Comment