Mawakili wa upande wa
utetezi katika kesi ya kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza ugaidi
inayomkabili mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wamepinga
maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Adamu Kasekwa yasitolewe
mahakamani hapo kama kielelezo na Kamanda wa Polisi Kinondoni, Ramadhan
Kingai.
Hiyo ni kutokana na
maelezo hayo kuchukuliwa nje ya muda kisheria na sababu ya pili ni Kasekwa
kabla na wakati wa kuchukuliwa maelezo yake katika kituo kikuu cha Polisi Dar
es Salam, anadaiwa kuteswa na askari polisi chini ya usimamizi wa Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai.
Mapingamizi hayo
yametolewa leo Jumatano Septemba 15, 2021 na kiongozi wa Jopo la mawakili 14 wa
upande wa utetezi, Peter Kibatala katika Mahakama Kuu divisheni ya makosa ya
rushwa na uhujumu uchumi wakati Kingai ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa
mashtaka alipokuwa akitoa ushahidi wake.
Katika ushahidi wake,
Kingai ameieleza mahakama hiyo kuwa yeye ndio aliyehusika kuandika maelezo ya
onyo kwa Kasekwa, hivyo ameiomba mahakama hiyo iyapoke na kuwa sehemu ya
kielelezo katika kesi hiyo.
Ombi hilo lilipingwa
na upande wa utetezi kwa madai kuwa mteja wao alihojiwa nje ya muda wa kisheria
kwa sababu, Kasekwa alikamatwa Agost 5, 2020 Moshi Mmoani Kilimanjaro na
alihojiwa Agosti 7, 2020, hivyo kisheria mshtakiwa anapokamatwa anatakiwa
kuhojiwa ndani ya saa nne na si vinginevyo.
Kutokana na wakili
Peter Kibatala kuwasilisha mapingamizi hayo, wakili wa Serikali mwandamizi,
Robert Kidando amedai kuwa mapingamizi hayo yatatatuliwa na mahakama kwa
kusikiliza kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi.
Kutokana na hali hiyo,
Jaji Mustapha Siyani anayesikiliza shauri hilo, ameahirisha kesi hiyo kwa
muda hadi saa nane mchana, ambapo itakuja kwa ajili ya usikilizwaji wa kesi
ndogo kuhusu utaratibu wa utoaji wa maelezo ya onyo ya Kasekwa baada ya
mawakili wake kuyapinga wakidai kuwa aliyatoa baada ya kuteswa.
Katika ushahidi wake,
Kingai ameieleza mahakama hiyo kuwa Julai 2020 alipigiwa siku na aliyekuwa DCI,
Robert Boaz alimtaka afike ofisini kwake na yeye aliitikia wito huo.
Akiwa katika ofisi
hiyo, alitambulishwa kwa Luteni Denis Urio na kwamba Boaz alimueleza Kingai
kuwa, Urio ana taarifa muhimu ya uhalifu na alimwambia Luteni Urio awaeleze kwa
pamoja.
"Luteni Urio
alitueleza kuwa kuna kundi maalumu la kihalifu linaandaliwa na Freeman Mbowe na
lilikuw ana lengo la kudhuru viongozi wa Serikali na kundi hilo lilikuwa
limepanga kulipua vituo vya mafuta na masoko na kukata miti na kuweka
barabarani ili gari zisipite na kufanya uporaji.”
"Luteni Urio
alitueleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni nchi isitawalike katika kuelekea
uchaguzi mkuu uliokuwa unataka kufanyika na kwamba Urio alituambia kuwa Mbowe
alimuomba amtafutie makondo wa Jeshi ambao wamestaafu au waliofukuzwa
kazi" amedai Kingai.
Amedai kuwa vitendo
hivyo nilipangwa kufanyika katika maeneo ya Moshi, Arusha, Mbeya, Dar es Salaam
na Mwanza.
Shahidi huyo
ameendelea kudai kuwa baada ya kupewa taarifa hiyo, Luteni Urio aliambiwa na
Boaz aendelee kushiriki katika mpango huo na ashirikiane na Polisi kwa
kila kitu kinachoendelea katika mpango huo.
"Hivyo Luten Urio
alitakiwa kuripoti kwangu kwa kuwa mimi nilikuwa Kamanda wa Polisi wa
Mkoa wa Arusha kwa kipindi kile na kabla sijaondoka Dar es Salaam kwenda Arusha
katika kituo changu cha kazi, Boaz alinielekeza nifungue jalada la uchunguzi
kuhusiana na maelezo aliyotoa Luteni Urio," amedai.
Washtakiwa wengine ni
Halfan Hassan, Mohamed Lingw'enya na Freeman Mbowe
No comments:
Post a Comment