MTANZANIA MBARONI KWA UGAIDI KENYA

Wakati bado kukiwa na taharuki kutokana na tukio la mauaji ya watu watano wakiwemo askari polisi watatu lilitokea jirani na Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam, nchini Kenya vyombo vya usalama vinamshikilia raia wa Tanzania kwa tuhuma za ugaidi.

Mtanzania huyo ambaye mamlaka zimegoma kutaja jina lake, anashikiliwa akitajwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa wawili wa ugaidi waliokamatwa wakati wakiwa kwenye harakati za kushambulia vituo vya usalama na maduka makubwa mjini Mombasa.

Habari zinaeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika kivuko cha Likoni majira ya asubuhi.

Hata hivyo, Polisi wamegoma kuelezea kwa undani kuhusu watuhimiwa hao huku wakieleza kuwa wanaendelea na uchunguzi.

Kwa mujibu wa polisi, watuhumiwa hao wanadaiwa walikuwa na dhamira ya kushambulia vituo viwili vya polisi na duka kubwa maarufu katika eneo la Nyali.

Taarifa za kipolisi zinadai kuwa kulikuwa na mpango wa kutekeleza shambulio hilo leo katika kuadhimisha tarehe ya kifo cha Sheikh Aboud Rogo, ambaye aliuawa Agosti 27, 2012 kwa tuhuma ya kuhusika na ugaidi.

Taarifa zinaeleza kuwa watuhumiwa hao walizingirwa na wapelelezi kutoka Kikosi Maalum na Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU) walipokuwa kwenye gari aina ya Toyota Probox nambari KCE 695U kabla ya kutekeleza  shambulio hilo.

Maofisa hao waliwazingira na kuwavamia wawili hao wakati wakizozana na maofisa wa kivuko hicho kuhusu malipo ya kuvusha gari walilokuwa wakilitumia.

Baada ya kukamatwa waliingizwa kwenye gari la polisi huku wananchi wakishuhudia kisa hicho kama sinema. Mzozo ulitokea katika kivuko hicho wakati watuhumiwa hao walipogomea kufanya malipo kwa njia ya mtandao.

Mara baada ya kutiwa mbaroni, bunduki mbili za AK-47, simu za mkononi, risasi 150 na vitu vingine vilipatikana wakati maofisa hao wa usalama wakifanya upekuzi kwenye gari hilo la watuhumiwa.

Tayari watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani jijini Nairobi kujibu mashtaka yanayowakabili.

 

MTANZANIA MBARONI KWA UGAIDI KENYA MTANZANIA MBARONI   KWA UGAIDI KENYA Reviewed by KUSAGANEWS on August 26, 2021 Rating: 5

No comments: