Usikilizwaji wa kesi ya Uhujumu Uchumi
inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake wawili umekwama kwa
muda baada ya wanachama na wafuasi wa Chadema kugomea masharti yaliyowekwa na
mahakama kwa watu wanaotaka kuingia ukumbini kusikiliza kesi hiyo.
Mbowe na wenzake- Halfani Bwire Hassan, Adamu
Hassan Kasekwa na Mohamed Abdilkahi Ling'wenya wanatuhumiwa kujihusisha makosa
ya ugaidi na uhujumu uchumi.
Kesi hiyo namba 16 ya mwaka 2021 inasikilizwa
katika Mahakama Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,
Dar es Salaam.
Miongoni mwa masharti yaliyogomewa ni
kutoingia na simu katika chumba cha mahakama.
Pia mahakama imetoa utaratibu mpya wa kuingia
mahakamani hapo leo ambapo mawakili 20 wa utetezi, mawakili wa serikali nane,
ndugu wa washitakiwa wasiozidi watano, viongozi watano, watu wa ulinzi na
usalama watano, wanahabari 10 na watu maalumu watatu ndio watakaoruhusiwa
kuingia kwenye ukumbi wa mahakama.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mustapha
Siyani likuwa imepangwa kuendelea leo Alhamisi Septemba16, 2021 kuanzia saa
4:00 asubuhi.
Mpaka sasa kesi hiyo haijaanza kusikilizwa
ingawa washtakiwa walikuwa wameshaingizwa mahakamani pamoja na mawakili wa
pande zote. Wakati wakimsubiri jaji, tangazo likatolewa likiwataka watu wote kutoka
nje na wabaki washtakiwa tu.
Baada ya watu wote kutolewa nje wakiwamo
washtakiwa ambao walirudishwa mahabusu, hakuna taarifa yoyote ya nini
kinachoendelea au kinachofuata.
Kwa sasa, hata waandishi ambao awali walikuwa
wameruhusiwa kuingia na simu wametakiwa waache nje.
No comments:
Post a Comment