Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais Tamisemi, Ummy Mwalimu, leo Ijumaa, Agosti 6,2021 ameagiza kusimamishwa
kazi kwa Mkuu wa idara ya elimu msingi wa Halmashauri ya jiji la Arusha Omary
Abdalahemedi Kwesiga kufuatia kufanya mzaha wa maigizo ya uchomaji sindano ya
chanjo ya Covid-19.
Hata hivyo Waziri Ummy
amemuagiza Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, kumchukulia hatua
muuguzi wa Hospitali ya Mount Meru Arusha, Scholastica Kanje.
Ummy ametoa maagizo
hayo leo Ijumaa, Agosti 6, 2021 siku moja baada ya video iliyosambaa mitandaoni
inawaonyesha wawili hao wakifanya kitendo hicho.
Taarifa iliyotolewa na
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini ofisi ya Rais Tamisemi, Nteghenjwa
Hoseah imeeleza kuwa kitendo hicho ni kinyume cha taratibu na kanuni za utoaji wa
huduma za chanjo na hivyo kuleta sintofahamu kwa wananchi.
“Kutokana na hali hiyo
Waziri wa Tamisemi amemuagiza Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tamisemi kumsimamisha
kazi mwalimu Omary Abdalahemedi Kwesiga pia ameagiza Scholastica Kanje ambaye
ni ofisa muuguzi msaidizi apelekwe kwenye baraza la uuguzi na ukunga kwa hatua
zaidi,” alieleza taarifa hiyo.
Mara baada ya agizo
hilo, Msajili wa baraza la uuguzi na ukunga Tanzania, Agnes Mtawa ametangaza
kumsimamisha kazi kwa miezi mitatu muuguzi wa Hospitali ya Mount Meru Arusha,
Scholastica Kanje.
Msajili amesema
Scholastica alifanya mzaha katika jambo hilo la kitaifa kwa kuigiza kumchoma
sindano mteja na kusambaa mitandaoni suala linaloweza kuleta upotoshaji mkubwa
na kuzua taharuki kwa wananchi.
“Kitendo hiki ni kinyume cha sheria ya uuguzi
na ukunga ya mwaka 2010 (25)(3)(k) na maadili ya ukunga na uuguzi inayomtaka
kila muuguzi afanye kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa na viwango.
“Kutokana na kitendo
hicho nimemuagiza muuguzi mkuu wa mkoa ambaye ni msimamizi wa taaluma katika
mkoa kumsimamisha kazi kwa kipindi cha miezi mitatu na kisha kutoa taarifa ya
zoezi zima la lililosababisha muuguzi huyu kufanya mzaha huo ambayo
itawasilishwa kwenye kikao cha baraza kwa maamuzi,” amesema Mtawa.
No comments:
Post a Comment