Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu wamesomewa upya mashtaka sita yakiwemo ya kufadhili vitendo vya ugaidi na kukusanya pesa kwa kufanya vitendo vya kigaidi.
Mashtaka mengine ni kukusanya fedha kwa ajili ya kufanya vitendo
vya kigaidi, kukutwa na silaha aina ya bastola na kukutwa na sare za jeshi
kinyume cha sheria.
Kati ya mashtaka hayo sita, Mbowe anakabiliwa
na mashtaka mawili ambayo ni kula njama na kufadhili fedha kwa ajili vitendo
vya kigaidi.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo
Ijumaa, Agosti 6, 2021 na jopo la mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas
Simba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Akiwasomea mashtaka hayo, wakili Hilla amedai kuwa washtakiwa
wanakabiliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 63/2020.
Amedai katika kosa la kwanza, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa
kula njama za kutenda kosa, tukio wanadaiwa kulitenda kati ya Mei Mosi, 2020 na
Agosti Mosi 2020 katika hoteli ya Aishi iliyopo Wilaya ya Moshi mkoani
Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, Morogoro na
Arusha, walitenda kosa hilo.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa walikula njama za kulipua vituo
mbalimbali vya mafuta na katika mikutano isiyokuwa ya kisiasa na kusababisha
hofu kwa wananchi kwa lengo la kuutishia umma wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania .
Shtaka la pili ni kufadhili vitendo vya kigaidi, linalomkabili
Mbowe ambapo anadaiwa katika tarehe hizo, katika hoteli ya Aishi iliyopo
Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es
Salaam, Morogoro na Arusha, Mbowe aliwafadhili Halfan Hassan, Adam Kasekwa na
Mohamed Lingwenya, huku akiwa na lengo la ufadhili huo utatumikia katika
kutekeleza vitendo vya kigaidi ambavyo ni kulipua vituo ya mafuta na mikusanyiko
ya wananchi.
Mbali na Mbowe, ambaye ni mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo,
washtakiwa wengine ni Halfan Hassa, Adam Kasekwa na Mohamed Lingwenya.
Washtakiwa baada ya kusomewa amshtaka hayo hawakutakiwa kujibu
chochote na Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 13, 2021
itakapotajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande, kutokana mashtaka
yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Washtakiwa walikuwa wanatetewa na jopo la mawakili, tisa
wakiongozwa na Peter Kibatala.
No comments:
Post a Comment