Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Wilson Mahera leo Ijumaa Novemba 27, 2020 amesema katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alimuandikia barua Novemba 19, 2020 yenye orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum na kwamba tume hiyo ilitumia orodha hiyo kuteua wabunge wa viti hivyo.
NEC imeeleza hayo wakati kikao cha
kamati kuu ya Chadema kikifanyika leo jijini Dar es Salaam kuwajadili wanachama
wao 19 ambao Novemba 24, 2020 waliapishwa kuwa wabunge wa viti maalum mjini
Dodoma jambo lililopingwa na chama hicho na kueleza kuwa hakikuyapitisha
majina yao na kuitaka tume hiyo kusema ukweli.
Baada ya wanachama hao
kuapishwa, Mnyika alifanya mkutano na wanahabari na kueleza kuwa hakuna kikao
kilichokaa na kupitisha majina hayo na kuyapeleka NEC lakini leo tume hiyo
imemtaja Mnyika kuwa aliwasilisha majina hayo.
Katika taarifa yake kwa umma, Mahera
amesema, “ifahamike kwamba katibu mkuu wa Chadema alimuandikia mkurugenzi wa
NEC barua yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/20/TU/05/141 ya Novemba 19
ambayo iliwasilisha orodha ya majina ya wanachama wanaopendekezwa kuteuliwa
kuwa wabunge wa viti maalum.”
“Tume ilitumia orodha
iliyowasilishwa na Chadema kuteua wabunge wa viti hivyo. Hivyo, wabunge
wanawake wa viti maalum wa Chadema waliteuliwa kwa kuzingatia taratibu zote za
kikatiba na kisheria.”
Mahera amesema kuanzia Septemba 26,
tume hiyo imekuwa ikipokea barua kutoka kwa vyama mbalimbali zenye mapendekezo
ya wanawake wabunge na madiwani wa viti maalum.
“Septemba 26 tume ilipokea
kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM) na Novemba 19 ilipokea kutoka Chadema.
Mapendekezo ya wabunge wanawake wa viti maalum kwa Chadema yaliwasilishwa tume
kwa barua.”
“Mnamo Novemba 20 tume katika kikao
chake iliteua wabunge na madiwani wanawake wa viti maalum kwa kuzingatia
matakwa ya katiba na sheria,” alisema Mahera huku akieleza kuwa si kweli
kwamba tume iliteua wabunge wa Chadema ambao majina yao hayakuwasilishwa
kwa kuzingatia taratibu.
No comments:
Post a Comment