Jeshi la polisi mkoani Arusha limefanikiwa kukamata mtandao wa watuhumiwa watatu wa mauaji ya matukio ya wanawake mkoani Arusha ambayo yamekuwa yakifanyika mara kwa mara.
Akizungumza na
waandishi wa habari mkoani Arusha leo Jumatatu Februari 15 Kamanda wa polisi
mkoani Arusha,Salum Hamduni aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mbise Sanare
Lekumo(30) mkazi wa Olasiti ,Lembeka Olomorojo(65) mkazi wa Osunyai na mganga
wa kienyeji Bashiri Msuya (64)mkazi wa mtaa wa Kirika B kata ya Osunyai jijini
Arusha.
Hamduni alisema kuwa,
watuhumiwa wote kwa pamoja walihusika katika mauaji ya mwanamke mmoja
aliyejulikana kwa jina la Anna Edward(44) mkazi wa kata ya Mateves lilitokea
Januari 25,2021 .
Aidha Kamanda alisema
kuwa, watuhumiwa kwa pamoja walimwua mwanamke mwingine aitwaye Stella Daniel
(22) katika tukio lililotokea Mei 21 ,2019 katika eneo la Lolovono, huku tukio
lingine likiwa ni mauaji ya mwanamke mwingine aitwaye Bahati Prosper (35)
lililotokea Januari 16,2020 katika eneo la Ngaramtoni ya chini .
Kamanda alisema kuwa,
matukio hayo yote yalisababisha baadhi ya wanawake kuandamana na kufunga
barabara Januari 30 ,2021 ikiwa ni njia ya kufikisha malalamiko yao kwa
serikali ,hali iliyomsababisha kuomba muda na kufanyia kazi malalamiko yao ya
tukio hilo la mauaji.
Kamanda alisema kuwa,
baada ya kuwahoji watuhumiwa hao walikiri kuhusika na matukio hayo na kuwa
sababu zimetajwa kwamba ni imani za kishirikina na kuwa baada ya upelelezi kukamilika
jalada litapelekwa ofisi ya Taifa ya mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.
Wakati huohuo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na
Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya kaskazini kilicho chini ya Mamlaka ya
usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA) na vyombo vingine vya ulinzi na
usalama kwa kipindi cha mwaka 2010/2020 kwa pamoja walifanikiwa kukamata
silaha 126 Kati ya hizo Magobore ni 125 na Semi Automatic Rifle Moja zikihusika
na makosa dhidi ya wanyamapori.
Kamanda alisema kuwa ,
watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani na kuhukumiwa na silaha hizo
kutaifishwa.
"Baada ya taratibu
zote za kisheria kukamilika silaha zote zinatarajiwa kupelekwa makao
makuu ya Jeshi la Polisi kwa ajili ya taratibu za kuharibiwa ili zisiweze
kuingia Tena kwenye shughuli za kihalifu ikiwa ni pamoja na mitandao ya
ujangili," amesema Kamanda.
Hata hivyo, ametoa wito
kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi la polisi ,kikosi
dhidi ya ujangili na vyombo vingine vya usalama ili kuwafichua wahalifu
wanaojihusisha na ujangili na hata wanaoingia katika hifadhi zetu bila
utaratibu ili hifadhi hizo ziendelee kuwa salama.
Naye Mkuu wa Kanda ya
kaskazini kikosi dhidi ya ujangili (KDU) ,Mbanjoko Manyenga amesema
kukamatwa kwa silaha hizo ni sehemu ya mkakati ya kupunguza ujangili nchini kwa
kushirikiana na jeshi la polisi hasa katika maeneo ya mapori Tengefu ambapo
ujangili wa wanyamapori umekuwa ukifanywa dhidi ya kitoeo.
No comments:
Post a Comment