Upande wa mashtaka katika kesi ya
uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzania, Erick
Kabendera umempa pole, baada ya kufiwa na mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi.
Mbali na kumpa pole, Serikali ya
Tanzania imepinga maombi ya upande wa utetezi ya kutaka mshtakiwa huyo
aruhusiwe kesho Ijumaa Januari 3, 2020 kwenda kushiriki Ibada ya mazishi ya
mama yake katika Kanisa Katoliki la Chang'ombe, jijini Dar es Salaam.
Kabendera anakabiliwa na mashtaka
matatu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambayo ni
kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh.173 Milioni
katika kesi ya uhujumu namba 75/2019.
Leo Alhamisi, Januari 2, 2020 Wakili
wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ametoa pole hizo wakati kesi hiyo
ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Simon aliieleza Mahakamani hiyo
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega kuwa Serikali ya
Tanzania inampa pole Kabendera kwa kufiwa na mama yake mzazi.
"Hata sisi tuna masikitiko
makubwa na tunampa pole nyingi Kabendera kwa kufiwa na mama yake mzazi, lakini
mahakama isifungwe mikono kwa maombi yaliyowasilishwa ya kutaka mshtakiwa
kushiriki msiba," amedia Wankyo.
Akijibu hoja za upande wa utetezi,
Wankyo amedai maombi ya Kabendera kupitia mawakili wake yamewasilishwa wakati
ambao si sahihi kwa sababu mahakama haina mamlaka na pia Mkurugenzi wa
Mashitaka (DPP) hajaipa kibali mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.
"Mheshimiwa hakimu katika macho
ya kisheria mahakama yako haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwa sababu
kesi hii ni ya uhujumu uchumi, licha ya kuwa hata sisi tuna masikitiko makubwa
lakini tunaiomba mahakama yako isifungwe mikono," amedai
Awali, Jebra Kambole aliwasilisha
mahakama ombi la kuiomba mahakama ya Kisutu imruhusu Kabendera akashiriki ibada
ya kumuaga mama yake mzazi katika Kanisa la Roman Katoliki lilipo Changombe,
wilaya ya Temeke majira ya mchana, huku akiwa chini ya ulinzi.
Kambole ameieleza mahakama kuwa
suala la kushiriki sala ya mwisho ya msiba ni haki ya msingi ya binadamu na ni
haki ya faragha na ni haki ya kuheshimu familia.
"Kushindwa kuhudhuria maziko ya
mama yake tutakuwa tumemuadhibu adhabu kubwa tena kwa kuangalia uhusiano wa
mshitakiwa na mama yake mzazi kwani alikuwa akimuuguza na ni vizuri akatoa
heshima ya mwisho," amedai Kambole.
Amedai ni muhimu kwa Kabendera
kushiriki ibada ya kumuaga mama yake mzazi kwa sababu mama mzazi ni mmoja,
akifa anaagwa mara moja na kama kumzika anazikwa mara moja.
"Hivyo ni muhimu mshtakiwa
akahudhuria tukio hili la kibinadamu," amedai Kambole na kuongezea
"Jamhuri haitaathirika kwa
lolote kwa sababu mshitakiwa atakuwa chini ya ulinzi na ibada itakuwa mchana
kanisani na Temeke sio mbali na gerezani, tunaomba akatoe heshima ya
mwisho," ameomba.
Baada ya kutoa hoja hizo, Hakimu
Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi kwa muda hadi saa 8:45 mchana wa leo Alhamisi,
ambapo atatoa uamuzi kama Kabendera ashiriki Ibada ya mazishi ya mama yake
mzazi au laa.
Mama wa Kabendera alifariki dunia
Jumanne ya wiki hii Desemba 31, 2019 katika Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini
Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa siku mbili kwa ajili ya matibabu.
Serikali yampa pole Erick Kabendera kufiwa na Mama yake Mzazi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
January 02, 2020
Rating:
No comments:
Post a Comment