Wameshiriki kweli aise! Hiyo ni kati ya kauli zinazoweza
kuwa zimetolewa na watu baada ya kumwona Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani
nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe akiingia ndani ya uwanja wa CCK
Kirumba jijini Mwanza kuhudhuria maadhimisho ya Kitaifa ya miaka 58 ya Uhuru wa
Tanganyika.
Hata hivyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu
hawakuvaa sare maalum za chama wala kombati ambazo zinatumiwa kama vazi maalum
chama chao lakini wamepigilia suti nyeusi, mashati meupe na tai.
Uwanjani pia hawajaonekana wananchi waliovaa sare wala
vazi linaloonekana kama alama ya Chadema tofauti na wenzao wa CCM ambao baadhi
yao wamevaa sare rasmi za chama za rangi ya kijani na njano.
Akiwa ameongozana na Nyalandu aliyewahi kuwa waziri wa
maliasili na utalii wa Tanzania, Mbowe ameingia uwanjani kupitia lango la
viongozi wa kitaifa na kupokelewa kwa heshima zote kama ilivyofanyika kwa
viongozi wengine.
Baada ya kupokelewa, Mbowe na Nyalandu wameongozwa moja
kwa moja na kuonyeshwa eneo la kuketi katika jukwaa kuu waliko viongozi wengine
wa kitaifa wa sasa na wastaafu.
Kushiriki kwa Mbowe kwenye maadhimisho ya mwaka huu
kumehitimisha ‘mgomo’ wa karibia miaka minne tangu mwaka 2015 wa Chadema na
viongozi wake kususia kushiriki maadhimisho ya kitaifa.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Itikadi na Uhusiano wa Umma
wa Chadema, John Mrema aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana
Jumapili Desemba 8, 2019 kuwa chama hicho kimetafakari na kuamua kushiriki
maadhimisho ya mwaka huu kwa sababu kinajiandaa kushika Dola.
“Ni kweli tangu Serikali ya awamu ya tano iingie
madarakani hatujawahi kushiriki sherehe za Uhuru. Tumezingatia mambo mbalimbali
miongoni ni kwamba sisi ni chama kinachojiandaa kushika Dola na kwa sababu za
nyakati na muda ambao tupo, tumeamua kushiriki,” alikaririwa Mrema
“Kwa miaka mitatu tumekuwa tukishauriana ndani ya chama,
nje ya chama na wadau mbalimbali. Kama chama tumefanya uamuzi wetu tunaamini ni
sahihi na baadaye tutawaeleza wanachama wetu kwa kina na mapana,” aliongeza
Mbowe, Nyalandu walivyoingia maadhimisho miaka 58 ya Uhuru
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 09, 2019
Rating:
No comments:
Post a Comment